ASKOFU wa Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Frederick Shoo amewataka watanzania kuwaondoa katika moyo aliowaita "wapangaji wabaya", akihadharisha hata ukiwa na mali nyingi na maarifa mengi, kama unao wapangaji hao "ni kazi bure".
Amesema matokeo yake si furaha, ni kuishia kwenye uchungu, kukata tamaa na kuchukiana.
Dk. Shoo alikuwa akizungumza jana katika ibada ya sikukuu ya Krismasi iliyofanyika Kanisa Kuu la Usharika wa Moshi Mjini (Cathedral).
Katika mahubiri yake, Askofu Dk. Shoo alisema: "Toa wapangaji wabaya moyoni mwako, ambao wanamzuia Yesu asiingie na asiwe na nafasi katika maisha yako yote.
"Iwe ni kiburi, iwe ni majivuno, iwe ni uchoyo, iwe ni ubinafsi, iwe ni tabia mbaya za kumchukiza Mungu. Hawa ni wapangaji wabaya umewaweka katika moyo wako.
"Inawezekana hata kukosa imani ya kweli kwa Mungu umwaminie. Mali nyingi, maarifa mengi, kama umeweka wapangaji wabaya inakuwa ni kazi bure. Matokeo yake ni si furaha, ni kuishia kwenye uchungu, kugombana, kukata tamaa na kuchukiana."
Zaidi Askofu Dk. Shoo alionya kuwa pasipo Yesu, hayo yote wanayokumbatia, hatma yake ni uchungu na kuangamia.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED