JUMLA ya timu nane tayari zimefanikiwa kutinga hatua ya 32 Bora ya mashindano ya Kombe la Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF Cup) inayoendelea visiwani hapa.
Timu hizo ni pamoja na Union Ring, Super Star, Taifa Jang’ombe , Zafsa FC, Urafiki SC, Negro United, Sharp Boys na Kikungwi Star.
Hatua ya awali ya mashindano hayo ilishirikisha timu kutoka Ligi za mikoa mitatu ya Unguja na Ligi Daraja la Kwanza (Unguja).
Akizungumza na gazeti hili jana, Katibu wa Kamati ya Mashindano ya ZFF, Ali Bakari 'Cheupe', alisema ratiba ya mzunguko huo wa kwanza inatarajiwa kukamilika kesho kwa kupata timu 20 zitakazotinga hatua ya 32 Bora.
Bakati alisema katika kuhakikisha mzunguko wa pili unakuwa na mafanikio makubwa, kamati yake inaendelea na jitihada za kutafuta wadhamini ili kusaidia michuano hiyo kuwa na ushindani zaidi.
“Bado hatuna udhamini wa moja kwa moja wa mashindano haya katika hatua ya awali, japo tunaudhamini wa zawadi kwa bingwa tu kutoka katika Benki ya PBZ, hivyo tunawakaribishwa wadau kudhamini mashindano haya,” Cheupe alisema.
Mashindano hayo ya FA yanachezwa kwa kanda mbili (Unguja na Pemba) na mshindi wa Kanda ya Unguja atakutana na mshindi kutoka Pemba kupata bingwa ambaye ataiwakilisha Zanzibar katika michuano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED