KIUNGO mshambuliaji wa Simba, Jean Ahoua na Feisal Salum 'Fei Toto' wa Azam FC, wanaongoza kwa kufunga mabao ya penalti katika mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu inayoendelea.
Wachezaji hao wamefunga mabao matatu kwa njia hiyo, wakiwa hawajapoteza hata penalti moja waliyopewa dhamana ya kupiga.
Ahoua alitimiza bao la tatu kwa njia ya tuta alipofunga na kuipa Simba ushindi wa bao pekee katika mechi dhidi ya JKT Tanzania iliyochezwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam juzi.
"Hii siyo ya kwangu peke yangu, ni ushindi wa timu nzima, kila mmoja amechangia kupata ushindi, nafikiri tufurahi leo (juzi), tumepata pointi tatu, tutaangalia mechi ijayo," alisema Ahoua.
Rekodi za dawati la michezo Nipashe zinaonyesha kiungo mshambuliaji huyo ambaye ni raia wa Ivory Coast, alifunga mabao mengine ya penalti dhidi ya Dodoma Jiji, Simba ikishinda pia bao 1-0, nyingine dhidi ya KMC, akiiwezesha timu yake kushinda mabao 4-0.
Kwa upande wa Fei Toto, penalti zake alizifunga katika mchezo kati ya Azam FC dhidi ya KenGold, ikishinda mabao 4-1, dhidi ya Kagera Sugar ikiipa timu yake ushindi wa bao 1-0, na dhidi ya Dodoma Jiji, Wanalambalamba wakishinda mabao 3-1.
Wachezaji wanaofuatia kwa kufunga mabao mengi ya penalti ni, Leonel Ateba wa Simba, Erasto Nyoni wa Namungo na Morice Chukwu wa Tabora United.
Ateba alifunga katika mechi ambayo Simba ilitoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Coastal Union, na Pamba Jiji likiwa ni bao pekee kwenye mchezo huo.
Morice alifunga penalti zake kwenye mchezo ambao Tabora United ilishinda bao 1-0 dhidi ya Pamba Jiji na dhidi ya Mashujaa, ikishinda pia bao 1-0.
Wakati huo huo, Fei Toto ndiye kinara wa 'asisti' mpaka sasa kwenye Ligi Kuu, akiwa ametoa pasi saba za mwisho.
Kiungo mshambiliaji huyo anafuatiwa na Salum Kihimbwa wa Fountain Gate FC ambaye ana 'asisti' tano, huku Ahoua, Josephat Bada wa Singida Black Stars wote wakiwa na 'asisti' nne, pamoja na Stephane Aziz Ki, ambaye kabla ya mchezo wa jana kati ya Yanga dhidi ya Dodoma Jiji naye alikuwa na idadi hiyo ya pasi za mabao.
Ligi Kuu Bara inatarajia kuendelea tena leo kwa Tanzania Prisons dhidi ya Pamba Jiji itakayochezwa kwenye Uwanja wa CCM Sokoine jijini, Mbeya huku kesho Azam FC ikiwaalika JKT Tanzania.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED