Celestine aonesha njia yajayo BAWACHA

By Pilly Kigome , Nipashe
Published at 07:01 PM Dec 24 2024
Celestine Simba
: Pilly Kigome
Celestine Simba

MGOMBEA wa nafasi ya Uenyekiti Baraza la Wanawake Chadema (BAWACHA), Celestine Simba, amekuja na maazimio 12 ya kutaka kulibadilisha baraza hilo liwe imara na kuleta tija kwa wanawake nchini.

Akiongea na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam, leo, Desemba 24, 2024, amesema Baraza hilo linatakiwa liwe na mabadiliko makubwa katika kuliimarisha na liwe imara na kuleta tija kwa wanawake katika ushirikiano na uwajibikaji.

“Kwa miaka yote nimejikita katika kutetea haki za wanawake na kupitia mafunzo, mikutano na kampeni nimehamasisha wanawake wa mijini na vijijini kuhusu kujitambua na kushiriki maendeleo ya uchumi na kisiasa.

“Ninaamini kwa nafasi ya Uenyekiti wa BAWACHA ni jukwaa la kuniongezea uwezo wa kushirikiana na wanawake wote wa CHADEMA katika kuimarisha sauti zetu katika kuleta mabadiliko chanya na kuhakikisha wanashirikishwa kikamilifu katika siasa na maendeleo ya nchi,” amesema Simba.

Simba amesema dhamira yake ni pamoja na kuimarisha muundo wa BAWACHA, ili  kuwa na baraza lililojipanga vizuri, lenye uwazi, ushirikiano na tija katika kila ngazi, kuwezesha wanawake kiuchumi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kuanzisha program za kuwajengea uwezo wanawake kiuchumi.

Pia alisema ataimarisha uhamasishaji wa haki za wanawake, kushirikiana na makundi mengine, kuinua sauti za wanawake katika maamuzi ya chama, maboresho ya bodi ya maadili ya BAWACHA, uimarishaji wa ushirikiano wa kimataifa, mapambano ya haki za wanawake, vijana na watoto.

Ameongeza kwamba ataimarisha makongamano na miundombinu ya baraza, madai ya Katiba mpya na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi na kuimarisha Baraza la Wanawake Zanzibar.