Polisi yakamata mabasi manne yaliyozidisha abiria

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:48 AM Dec 25 2024
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Richard Abwao.
Picha:Mtandao
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Richard Abwao.

JESHI la Polisi Mkoa wa Tabora limekamata mabasi manne yanayodaiwa kuzidisha abiria katika doria zake za kipindi hiki cha msimu wa sikukuu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Richard Abwao, akitoa taarifa kwa waandishi wa habari jana ofisini kwake, alisema wanaendelea kufanya operesheni kabambe kuwasaka wahalifu na wavunjaji sheria.

Alisema kuwa katika kipindi hiki cha msimu wa sikukuu, kuna ongezeko la watu kuingia na kutoka katika mkoa huo, hivyo wanaendesha doria katika maeneo mbalimbali kuwasaka wahalifu na kufanya mkoa kuendelea kuwa salama.

"Tunafanya doria kwa kutumia askari wetu wenye magari, mbwa na wa miguu na tumefanikiwa kukamata mabasi manne yaliyozidisha abiria.

"Kitendo hiki ni cha uvunjifu wa sheria na kinahatarisha usalama wa abiria na mali zao, hivyo tutaendelea kufuatilia magari yote katika kipindi hiki na wakati wote," alisema.

Kamanda huyo alisema ametoa maelekezo kwa askari wa kata zote kusimamia vikundi vya ulinzi shirikishi ili kulinda amani na usalama wa watu katika maeneo yao, akisisitiza kuwa wamejipanga kutoa ulinzi wa kutosha katika nyumba za ibada na makazi hasa kipindi hiki cha sikukuu.

Aliwata watakaohitaji kupiga fataki kwenda kuchukua vibali na maelekezo ya jinsi ya kupiga, akiwaonya wenye tabia za kuchoma vitu barabarani na kufanya fujo na uharibifu kwamba watakamatwa.

Kamanda huyo pia aliwahimiza madereva kutotumia vilevi wakiwa wanaendesha magari wakati wote na kuzingatia sheria za usalama barabarani.

"Wamiliki wa kumbi za starehe wachukue tahadhari kwa kuhakikisha kunakuwa na hewa ya kutosha, kuchukua watu kwa idadi isiyozidi uwezo wao na kuwa makini wakati wote kwa kuwafuatilia watoto wote waliomo ndani ya kumbi na muda wa kumaliza na kutoka ni saa 12:00 jioni ili wawahi majumbani," aliagiza.