WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Dk. Ashatu Kijaji, amewataka wananchi wanaojihusisha na shughuli za uvuvi wa samaki kulinda rasilimali hizo ili wawekezaji waliowekeza viwanda vya kuchakata samaki wapate malighafi za kutosha.
Alitoa rai hiyo juzi baada ya kutembelea kiwanda cha kuchakata samaki cha Pride of Nile PVT Ltd kilichoko wilaya ya Muleba, mkoani Kagera.
Dk. Ashatu alisema ili uwekezaji huo uwe na matunda yanayotokana na juhudi za serikali za kuimarisha mazingira bora na wezeshi sambamba na kuhamasisha sekta binafsi, kuna umuhimu kulinda rasilimali za samaki na hivyo kupanua wigo wa kuongeza thamani ya mazao ghafi ya sekta za uzalishaji, ikiwamo uvuvi.
"Jukumu letu kama watanzania kwa sasa ni kuzilinda rasilimali hizi za asili kwa wivu mkubwa kwa sababu mbali na kutupatia ajira na kipato kwa mtu mmoja mmoja, rasilimali hizi pia zinanufaisha uchumi wa nchi kwa ujumla," alisema.
Dk. Ashatu pia alitoa rai kwa wananchi kuongeza nguvu kwenye ufugaji samaki kwa njia ya vizimba ili kupumzisha shughuli za uvuvi wa asili na kuwapatia nafasi samaki wa asili (wild fish) kuzaliana kwa wingi.
"Ninakuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuongeza kasi ya uhamasishaji ufugaji samaki kwa vizimba," alielekeza.
Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Dk. Abel Nyamahanga, alisema asilimia 70 ya eneo la wilaya hiyo limezungukwa na maji ya Ziwa Victoria na hivyo kufanya sehemu kubwa ya wakazi wake kuwa wavuvi, jambo linalowafanya kuwa na kila sababu ya kulinda rasilimali za ziwa hilo kwa nguvu kubwa.
Awali akisoma taarifa ya mchango wa kiwanda chao kwenye soko la ajira, Meneja Ubora wa kiwanda hicho, Hamza Mustapha alisema kimeajiri watanzania 125 na wanachangia uchumi wa taifa kwa kulipa mrabaha na kodi mbalimbali za serikali.
Hamza alisema upatikanaji mdogo wa malighafi hususani samaki aina ya sangara unasababisha kiwanda hicho kutumia chini ya asilimia 50 ya uwezo wake uliosimikwa.
"Tunaomba serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi ije na mkakati shirikishi wa kuhakikisha kunapatikana sangara wa kutosha kwa ajili ya kulisha viwanda ili kukuza mauzo nje na kulingizia taifa fedha za kigeni," alisema.
Dk. Kijaji baada ya kuapishwa, amekuwa ziara katika mikoa ya Kanda ya Ziwa. Tayari ameifikia mikoa ya Mara, Mwanza na Kagera, akilenga kufuatilia ufanisi wa sekta, kusikiliza na kupokea changamoto na mapendekezo ya wadau.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED