Serikali yavalia njuga ufaulu masomo ya Sayansi, Hisabati na Tehama

By Grace Mwakalinga , Nipashe
Published at 05:53 PM Jan 27 2025
Mratibu wa Mafunzo kupitia  Mradi wa Kuimarisha Elimu ya Sekondari nchini (SEQUIP) kwa Kituo cha Arusha, Majaliwa Mkalawa akifungua mafunzo hayo kwa Walimu na Wathibiti Ubora masomo ya Sayansi, Hisabati na Tehama kutoka mikoa ya Kilimanjaro na Arusha.
Picha: Grace Mwakalinga
Mratibu wa Mafunzo kupitia Mradi wa Kuimarisha Elimu ya Sekondari nchini (SEQUIP) kwa Kituo cha Arusha, Majaliwa Mkalawa akifungua mafunzo hayo kwa Walimu na Wathibiti Ubora masomo ya Sayansi, Hisabati na Tehama kutoka mikoa ya Kilimanjaro na Arusha.

WIZARA ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, imesema hatua madhubuti zinachukuliwa ili kuboresha ufaulu wa masomo ya Sayansi, Hisabati na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) nchini.

Katika juhudi za kuimarisha Elimu, Wizara imeeleza kuwa walimu wa masomo hayo wanapatiwa mafunzo ya kila mara, kwa lengo la kuboresha ufanisi wao katika ufundishaji na ujifunzaji.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo maalum kwa walimu wa masomo ya Sayansi, Hisabati na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), kutoka  mikoa ya Arusha na Kilimanjaro, Mratibu wa Kituo cha Arusha, Majaliwa Mkalawa, alisema kuwa ni sehemu ya jitihada za serikali katika kuhakikisha kuwa taifa linakuwa na wataalamu bora katika sekta ya Sayansi na Teknolojia.

Alisema kuwa, kupitia Mradi wa Kuimarisha wa Elimu ya Sekondari  nchini (SEQUIP), Wizara inatoa mafunzo maalum kwa walimu kazini ili kuwajengea uwezo wa kufundisha masomo hayo kwa ufanisi zaidi.

Alisema lengo la mafunzo hayo ni kuhakikisha kuwa walimu wanapata mbinu bora za ufundishaji, huku wakifundisha masomo ya Sayansi, Hisabati na Tehama kwa njia inayowavutia na kuwahamasisha wanafunzi.

“Wizara imedhamiria kuboresha ufundishaji wa masomo ya Sayansi, Hisabati na Tehama kwa walimu, ili kuongeza ufanisi wanafunzi kuyapenda masomo hayo na kufanya vizuri kwenye mitihani yao, hatua hizi zinatarajiwa kuchangia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo ya taifa, kwa kutoa wataalamu bora katika sekta ya Sayansi na Teknolojia, ambao wataweza kushughulikia vikwazo vya kiuchumi na kijamii,” alisema Mkalawa.

Ofisa Elimu Taaluma Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, Edith Chona akifungua Mafunzo ya Walimu wa masomo ya Sayansi, Hisabati na Tehama yanayofanyika katika Shule ya Sekondari Ilboru jijini Arusha.
Akizungumza kwa niaba ya Ofisa Elimu Mkoa wa Arusha, Ofisa Elimu Taaluma Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, Edith Chona, alisema mafunzo hayo yatawasaidia walimu kuboresha utendaji wao wa kazi.

Alisema walimu watapata mbinu za kisasa za ufundishaji, ambazo zitawasaidia kuwafundisha wanafunzi kwa njia ya kuvutia na inayoendana na mabadiliko ya kiteknolojia, hivyo wanafunzi watapenda masomo ya sayansi na kufanya vizuri kwenye mitihani.

Mwalimu wa somo la Baiolojia kutoka Shule ya Sekondari Ngarenaro iliyopo Arusha, Dilioza Assenga, alisema anatajia kujifunza mbinu mbalimbali zitakazomsaidia kufundisha wanafunzi kwa ufanisi.

Aliongeza kuwa  kwa  kutumia mbinu hizo, atawahamasisha wanafunzi, hususan wa kike, kuyapenda masomo ya sayansi na kuwawezesha kuwa wataalam katika fani mbalimbali baadaye maishani.

Zaidi ya walimu 500 na wathibiti ubora kutoka mikoa ya Arusha na Kilimanjaro wanapata mafunzo maalum ya Sayansi, Hisabati na Tehama katika Shule ya Sekondari Ilboru iliyopo jijini Arusha.