Polisi yatahadharisha abiria kuepuka kula ovyo

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:59 AM Dec 25 2024
Polisi yatahadharisha abiria kuepuka kula ovyo
Picha: Mtandao
Polisi yatahadharisha abiria kuepuka kula ovyo

JESHI la Polisi Wilaya ya Muheza, limetoa tahadhari kwa abiria wanaosafiri kwenda mikoani kipindi cha Sikukuu ya Krismasi na Mwaka Mpya wanaotumia mabasi kuwa waangalifu na matapeli.

Wito huo ulitolewa juzi na Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Wilaya ya Muheza, Leonard Bandola, wakati akitoa elimu kwa abiria katika mabasi yanayosafiri kwenda mikoani katika stendi kuu wilayani hapa.

Alisema, kipindi cha kuelekea Sikukuu ya Krismasi na mwaka mpya kumekuwa na matukio mbalimbali ikiwamo watu kutapeliwa fedha na mizigo katika mabasi.

Bandola alisema, abiria wanaopanda katika mabasi wasikubali kushirikiana na abiria mwingine kula chakula chochote hata tunda kwa kuwa wengine wanaweka dawa za kulevya ili kuwaibia abiria wakisisinzia ndani ya basi.

Katika hatua nyingine kamanda huyo aliwaasa abiria kutoa taarifa kwa polisi kutumia namba za polisi zilizopo katika mabasi hayo wakiona dereva anakwenda mwendo kasi ama kufanya uzembe wowote barabarani ikiwamo kuyapita magari mengine kwenye kona ama dereva kulewa.

Bandola alisema kuwa Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, limejipanga kudhibiti madereva kwenda mwendo kasi, walevi na wanaofanya makosa mbalimbali ya usalama barabarani.

Alisema pia jeshi hilo limejipanga kufanya doria za miguu, magari na pikipiki katika kipindi hiki cha sikukuu ili kudhibiti uhalifu na wakristo washerehekee sikukuu ya Krismasi na Mwaka Mpya kwa amani na utulivu wakiwa katika starehe, majumbani na nyumba za ibada.