STRAIKA Prince Dube, ambaye ni raia wa Zimbabwe amefikisha mabao matano huku akiiongoza Yanga kuisulubu Dodoma Jiji magoli 4-0 katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri Dodoma jijini, Dodoma jana.
Ulikuwa ni ushindi wa nne mfululizo kwa Yanga, tangu mara ya mwisho ilipofungwa mabao 3-1 dhidi ya Tabora United, mechi iliyofanyika Novemba Mosi, mwaka huu, ambapo baada ya hapo, iliichapa Namungo FC mabao 2-0, Mashujaa mabao 3-2 na Prisons mabao 4-0.
Dube amefikisha mabao matano kwa mechi tatu mfululizo alizocheza, akifunga 'ha-trick' katika mechi dhidi ya Mashujaa FC, kwenye ushindi wa mabao 3-2, bao moja dhidi ya Prisons, kabla ya jana kutimiza idadi hiyo ya mabao.
Mabao mengine ya Yanga katika mchezo wa jana yalifungwa na Clement Mzize ambaye amefikisha mabao manne wakati Stephane Aziz Ki, alifunga bao moja.
Ushindi huo umeifanya Yanga kuendelea kung'ang'ania katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, lakini ikiendelea kuifukuza Simba kileleni kwa kufikisha pointi 36, ikicheza mechi 14, ikiwa ni pungufu ya pointi moja dhidi ya vinara hao wenye pointi 37.
Aziz Ki, alianza kulitia msukosuko lango ya Dodoma Jiji dakika ya nne, baada ya shuti lake la mbali alilopiga kwa mguu wa kushoto kupita juu kidogo ya mwamba wa lango.
Dakika moja baadaye alifanya jaribio lingine la hatari, baada ya kona aliyopiga kugonga mwamba wa juu, kabla ya kukolewa na mabeki wa Dodoma Jiji.
timu mwenyeji.
Kama ingekuwa makini, Dodoma Jiji ingeweza kujipatia bao dakika ya sita ya mchezo, baada ya mabeki wawili wa Yanga, Ibrahim Hamad 'Bacca' na Nickson Kibabage kugongana wenyewe kwa wenyewe, ikampa nafasi Zidane Sereri kuuchukua kirahisi na kuondoka nao kwenye wingi ya kulia.
Hata hivyo, badala ya kumpa mwenzake Idd Kipagwile, aliyekuwa katika nafasi nzuri, aliamua kupiga mwenyewe akiwa kwenye 'engo' ngumu, mpira ukapiga nyavu na nje na kubaki akilaumiwa na wenzake.
Yanga ilipata bao la kwanza dakika ya 18, lililowekwa wavuni na Mzize, aliyeruka juu na kuunganisha kwa kichwa mpira wa kona uliopigwa na Pacome Zouzoua.
Bao hilo liliwafanya wachezaji wa Yanga wawe kama wametiwa ufunguo, kwa sababu waliendelea kuliandama kwa kasi lango la Dodoma Jiji ambao walionekana kuchanganyikiwa na kufanya makosa mengi yaliyowatia matatani muda mwingi wa mchezo huo.
Haikushangaza waliposababisha penalti ambapo kipa wake, Mohamed Hussein, alipolazimika kutoka langoni kwenda kukabiliana na Dube kutokana na uzembe wa mabeki wake, lakini alimfanyia madhambi na mwamuzi, Ahmed Arajiga, kutoka Manyara 'akafunika'. Penalti hiyo ilitiwa ndani ya kamba na Aziz Ki dakika ya 28 ya mchezo.
Alikuwa ni Mzize kwa mara nyingine tena alipopachika bao la tatu dakika ya 37 kwa shuti la mbali, baada ya kuona lango lipo tupu.
Kosa lililiofanywa na mmoja wa mabeki wa Dodoma Jiji kutoa pasi nyuma, badala ya kuwapasia wenzake ilionekana kwenda kwa Pacome, hivyo kipa, Hussein alilazimika tena kwenda kuokoa, lakini hakupata msaada kwa mabeki wake, Yanga wakaupora mpira na kabla hajarejea, Mzize aliupiga kwa mbali na kukwama wavuni.
Kipindi cha pili kila timu ilifanya mabadiliko ambayo kwa kiasi fulani yaliisaidia Dodoma Jiji kutokana na kuonekana wanaonana, huku Yanga ikipunguza kasi yake iliyoanza nayo kipindi cha kwanza.
Ni kipindi ambapo Dube alipopachika bao la nne kwenye mchezo huo, dakika ya 62 lililotokana na makosa ya wachezaji wa Dodoma Jiji walipojaribu kupasiana karibu ya eneo la hatari, lakini walinyanga'nywa na Aziz Ki aliyepiga shuti lililookolewa na kipa, mpira haukwenda mbali badala yake ulizua kizaazaa langoni kabla ya Dube kuukwamisha wavuni.
Dodoma Jiji imebaki na pointi 16, ikiwa nafasi ya 11, ikiwa imemaliza mechi zake 15 za mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED