MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Samia Suluhu Hassan ameelekeza masuala manne ya kutafakari na kufanyia kazi kwa viongozi wa chama hicho, ikiwamo kuzingatia miiko, kupinga dhuluma na uonevu wakati wa Uchaguzi Mkuu.
Mambo mengine ni tahadhari dhidi ya matumizi mabaya ya Akili Mnemba (AI) wakati wa uchaguzi, kuwaeleza wananchi namna serikali ilivyotekeleza ilani na kudumisha umoja.
Akifunga Mkutano Mkuu Maalumu wa siku mbili juzi jijini hapa, Rais Samia alisema viongozi wa CCM lazima waoneshe matendo mema na kuwa mfano bora wa kuigwa katika jamii kwa kupinga waziwazi dhuluma na uonevu na hujuma dhidi ya mambo mazuri yaliyomo nchini, ili kuwa na kauli thabiti kwa wanaotenda maovu.
"Kama sisi viongozi hapa, wewe ni mjumbe wa Mkutano Mkuu umetoka huko ulikotoka, wewe siyo mtu mdogo, hiki ndicho kikao cha juu kabisa cha chama chetu. Mkisema Kamati Kuu na Halmashauri Kuu laleni kwenye makapeti tutalala kwa sababu ninyi ni waajiri wetu
"Ukiwa mjumbe wa Mkutano Mkuu, cheo chako ni kikubwa sana, niwaombe sana tuendane na hadhi ya chama chetu, sisi sote wakati tunaomba kuwa wana-CCM tulitoa ahadi kwa chama hiki, zipo kwenye Katiba na kadi zetu, sifa na miiko ya kiongozi hasa tunapoelekea kwenye Uchaguzi Mkuu," alisema.
Aliongeza kuwa nchi ina uhuru mpana wa vyombo vya habari, hivyo wanapovitumia wawe makini wasitoe kauli zitakazosababisha utata kwa jamii na tafsiri isiyokusudiwa.
"Unaweza kusema jambo, sentensi yako ikawa na maudhui mchanganyiko, mwandishi asiye na nia njema akaamua kukata kipande kidogo cha yale uliyoyasema akayasambaza akakuharibia na kukitia doa chama chetu, niwaombe sana ndugu zangu umakini katika chama chetu," alisema.
Vilevile, alisema ukuaji wa teknolojia hasa Akili Mnemba, umekuja na mambo mengi, ikiwamo kuigiza sauti ya mtu na hata kusema mambo ambayo hajayasema.
"Tumeshuhudia kampeni kwenye nchi kubwa moja kule, tuliona mgombea mmoja anasemeshwa maneno kwamba anasema nikimshinda huyu atakwenda kuishi Zanzibar, Mama Samia mpokee huko mweke huko, huko Mama Samia wala hajulikani kihivyo, lakini ni matumizi ya Akili Mnemba," alisema.
Mwenyekiti huyo alisema kuwa mwaka huu wa uchaguzi anaamini matumizi ya teknolojia hiyo yatakuwapo na yanaweza kutumika vibaya kueneza uzushi na uchochezi.
"Pamoja na vyombo husika vikiendelea kuweka mikakati ya kushughulikia masuala haya ni vizuri, sisi wana CCM kujua hatari hiyo ili itakapotokea isitutoe kwenye mstari," alisema.
Mwenyekiti huyo pia aliwataka kudumisha umoja ndani ya chama na kwamba katika mchakato wa uchaguzi watakapopatikana wagombea, wawe wamoja ili kutafuta dola na kushinda.
Kuhusu utekelezaji ilani, Mwenyekiti Samia alisema wajumbe wa mkutano huo wana wajibu wa kueleza namna serikali ilivyotekeleza ilani ya uchaguzi kwa wananchi wa maeneo yao.
Pamoja na hayo, Mwenyekiti Samia aliwashukuru wajumbe kwa imani waliyoonesha kwake na Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Mwinyi na kwamba miaka mitano ijayo watakapochaguliwa watafanya zaidi.
"Lengo ni kuhudumia wananchi wetu na kuinyanyua nchi yetu kiuchumi, kisiasa na kijamii," alisema.
Akizungumzia kupumzika kwa Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango, Rais Samia alimshukuru kwa kazi kubwa aliyofanya ya kumsaidia kwenye sekta za kiuchumi kwa kuwa ni mchumi bobezi.
"Na alivyoomba kupumzika wakati ukifika tumwombe Mungu yale matamanio yake moyoni mwake yakatimie, apumzike vyema! Mungu ampe umri mrefu, afya njema na furaha ya moyo wake, tunakushukuru sana kwa utendaji kazi wako ndani ya taifa lako," alisema.
Aliwataja marais wastaafu (Jakaya Kikwete, Amani Abeid Karume na Dk. Ali Mohamed Shein) wamemsaidia kwenye mkutano huo kutokana na alivyoshtuka baada ya wajumbe kuja na hoja ya kutoa azimio la kuwapitisha kuwa wagombea wa urais yeye na Dk. Mwinyi kwenye Uchaguzi Mkuu mwaka huu.
"Nilipowaita chemba pia wamenisaidia sana, hapa niwashukuru sana na pengine nimshukuru Kikwete kwa sababu wazo hili lilikuja wakati yeye akiwa mwenyekiti wa chama, aliunda kamati ya wazee wa chama ambapo viongozi waliokuwapo wakikwama wanakimbilia kwao, wao ni ‘encropedia’ ya chama hiki, ukienda kwao hukosi ufumbuzi," alisema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED