Samia aonya majaji, mahakimu kujifanya miungu watu utoaji haki

By Paul Mabeja , Nipashe
Published at 09:42 AM Feb 04 2025
Rais Samia Suluhu Hassan akiteta jambo na Jaji Mkuu, Prof. Ibrahim Juma, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Sheria kitaifa, jijini Dodoma jana.

RAIS Samia Suluhu Hassan, amewataka majaji na mahakimu nchini, kuacha kuwa miungu watu katika utoaji wa hukumu na kuwataka watende haki kwa misingi ya sheria na Katiba ya nchi.

Pia, amewasihi wakati huu wanapoanza mwaka mpya wa mahakama, wazikague nafsi zao na dhamira kwa kudhamiria daima kukaa kwenye upande wa haki.

Rais Samia, alisema hayo jana jijini hapa, wakati akifunga maadhimisho ya Siku ya Sheria Tanzania, yaliyofanyika kwenye viwanja vya Chinangali.

“Niwakumbushe mwaka 1984 Mwalimu Julius Nyerere akihutubia kwenye mkutano wa majaji na makimu, aliwaasa watumishi kwa wakati huo kwa kuwaambia kwamba jaji au hakimu ni dhamana ambayo inataka uadilifu na nidhamu yako isitiliwe shaka hata kidogo hiyo ndio sifa ya kuwa jaji au hakimu.

“Nami niungane na kauli hiyo na niseme kwamba kazi ya kutoa haki ni kazi ya Mwenyezi Mungu, ambaye mbali na utoaji haki yeye ana jaala na kudra ambavyo pia huvitumia kumkadiria mwanadamu,” alisema Rais Samia.

Aidha, alisema majaji na mahakimu ni mawakala wa utoaji haki duniani, lakini wamenyimwa jaala na kudra na kwamba wanapaswa kufanya kazi zao kwa kufuata makubaliano ya Katiba na Sheria za nchi kama zilivyowekwa.

“Niwasihi sana, niwaombe sana tusiwe mungu watu hatuna sifa ya kudra wala jaala tutoe haki kwa misingi ile ambayo tumekubaliana na tumeiweka kisheria na kikatiba, niwasihi mnavyo anza mwaka mpya wa mahakama kagueni nafsi zenu na dhamira zenu daima chagua kukaa upande wa haki,” alisisitiza Rais Samia.

Aidha, alisema kutokana na kazi nzuri iliyofanyika hivi sasa kwenye haki jinai ipo haja ya kuweka nguvu kwenye upande wa haki madai.

Alisema kuwekeza nguvu kwenye haki madai kutasaidia serikali kutekeleza kwa ufanisi Dira ya Maendeeo ya Taifa ya Mwaka 2050.

Alisema ili kufanyika hilo mahakama pamoja na wadau wengine wanapaswa kujipanga kwenye utekelezaji wa dira hiyo.

Pia, alisema kutokana na uwekezaji kwenye haki jinai kwa mwaka 2024, jumla ya mashauri 172,301 yalisajiliwa na kumalizika kwa kutumia mfumo wa mtandao katika ngazi ya Mahakama za Mwanzo.

“Aidha, jumla ya mashauri 17,714 yalisikilizwa na kumalizika kwa njia ya mtandao katika mahakama za wilaya hadi mahakama kuu ambapo baadhi ya wadaiwa na mashahidi walitoa ushahidi wao kwa njia ya mtandao jambo ambalo hapo zamani ilikuwa kama ndoto,” alisema.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma, alisema migogoro ya ardhi imekuwa ni sehemu kuu inayozalisha mashauri ya jinai nchini.

Alisema kama eneo la ardhi litawekwa sawa litasaidia kupunguza mashauri ya jinai nchini, lakini pia kuipunguzia mzigo mahakama nchini.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari, alisema watafanya marekebisho ya sheria zote ambazo haziendani na Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050 ili zikidhi mahitaji ya sasa.

Hamza alisema ili Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050, ifanikiwe ipo haja ya kuboreshwa kwa sheria ili ziendane na kasi ya dira hiyo.

"Ili kufikia malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050 ipo haja kufanyika kwa maboresho ya sheria ili zikidhi matakwa na dira badala ya kukidhana," alisema Hamza.

Kadhalika, alisema katika kipindi cha kuanzia Julai hadi Desemba, mwaka jana, Sheria Kuu 300, zimefanyiwa tafsiri kutoka lugha ya Kingereza kwenda Kiswahili.

Naye Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Wakili Boniface Mwabukusi alisema chama hicho kitaendelea kujenga na kuimarisha ushirikiano na serikali, na kwa kufanya hivyo hawajalamba asali.

Mwambukusi, pia alisema wanaposhirikiana na serikali haimaanishi wamepewa rushwa ama pesa ili kuwafunga midomo.

Hata hivyo, alisema TLS sio kikundi cha magaidi bali ni 'Statutory body' (chombo cha sheria), katika sehemu za kuonya kitaonya na kupongeza kitapongeza kwa haki na kama kushiriki kazi za nchi kitashiriki pamoja ili kulijenga taifa na kumhudumia Mtanzania.