RIPOTI MAALUM:-1 Shuruba utafutaji wa mkaa, ahueni ya matumizi nishati safi

By Frank Monyo , Nipashe
Published at 09:08 PM Oct 22 2024
Mohamed Seif katika harakati zake za kusafirisha mkaa kwa wateja wake.
Picha: Frank Monyo
Mohamed Seif katika harakati zake za kusafirisha mkaa kwa wateja wake.

UNAPOUTAJA Mkoa wa Pwani, ni ulingo uliotawaliwa na utajiri na misitu ya asili. Lakini, upande wa pili matumizi ya utajiri huo omebeba ukakasi na madhila mengi.

Madhila hayo yanapotazamwa kwa wajasiriamali wa mkaa, ndilo kundi lenye madhara mengi, vikiwamo vifo, kama anavyosimulia aliyekuwa msafirishaji mkaa, Mohamed Seif:

"Mwaka 2022 mwishoni na mwanzoni mwa mwaka jana, nilipoteza rafiki zangu sita kutokana na ajali za pikipiki.

"Mimi pia katika kipindi hicho, nimepata ajali mara sita, nikaona ni heri niachane na hii kazi (kubeba mkaa porini), kwani ninategemewa na familia yangu na ndugu zangu."

Seif, ni kijana Ana familia ya watoto wawili walio katika umri wa chini ya miaka 10.

Ni mkazi wa Mlandizi, kitongoji cha Kwala, wilaya….mkoani….anamsimulizi kwa mwandishi wa makala hii.

Anasema mwishoni mwa mwaka 2022, alipata ajali zaidi ya sita, zikisababishwa na namna anavyoendesha pikipiki iliyobeba gunia za mkaa. Ubebaji ni wastani wa gunia tatu hadi nne. Kila moja lina kilo 150.

Seif, hajutii fedha anayoipata ingawa mazingira ya kazi hiyo yanampa vikwazo.

Miongozi mwa yanayomkuta n kuangukiwa na gunia aa mkaa. Sababu za ajali hizo zinajumuisha mwendokazi, kwanza kuwakimbia askari wa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS), utelezi kutokana na mvua.

"Ukimwona dereva wa pikipiki barabarani amebeba mkaa, ujue ana kilo 800, kwani gunia moja linakuwa na kilo kuanzia 150 hadi 250.

Hapo ukikuta dereva kapata ajali kwa kuangukiwa na mzigo, ana hatari kubwa ya kupoteza maisha akichelewa kupatiwa msaada," anasema.

Kijana huyo anasimulia yaliyomkuta katika harakati hizo, ikijumuisha kukohoa damu na kushindwa kupumua vizuri, akifafanua:

"Moja ya ajali niliyowahi kupata ambayo ilinisababishia kupumzika kazi hii, tulikuwa tunatoka porini eneo linaloitwa Kimara Misale Kwala (Halmashauri ya Chalinze, wilayani Bagamoyo).

Barabara ilikuwa mbovu kutokana na mvua, pikipiki yangu ilinizidi nguvu mzigo wa mkaa ukaniangukia na kunibana kifua.

Lakini nilipata msaada wa haraka ingawa niliumia sana eneo la kifua na kupelekea kulazwa Hospitali ya Tumbi (Kibaha).

Baada ya kukaa hospitalini kwa muda, nikaruhusiwa kurudi nyumbani, maisha yangekuwa magumu, lakini kitu kilichosaidia nilikuwa ninafuga kuku wa kienyeji, nawauza kupata fedha na kitoweo nyumbani."

Seif anasema alikuwa anafahamu kuwa ni kinyume cha sheria, lakini wazo lao lilitawaliwa na dhana ya 'riziki', waliamini na wenzake kwamba wakiendesha kinyemela porini wakiwa kundi la zaidi ya watu 40, itawasaidia.

Anasimulia maisha yake ya wakati huo, kwamba kabla ya kuanza safari ya kutoka porini na mzigo, na weznake waliwatuma wenzao wanaowaita 'surveyor' kwa maana ya wapelelezi, ambao wakiwahakikishia njia ni salama.

Ili kuwakadbili askari wa TFS, na kuanza safari kwa makundi, pikipiki zikiendeshwa kwa kasi na mazingira hatarishi kiafya.

Anasimulia chanzo kingine cha ajali ni kuwapo njia mbovu huko wanakofuata mkaa, hasa kipindi cha masika, akiwa na ufafanuzi wake "tunabeba gunia nne, tatu zinanyooshwa - zile ndefu - na moja linakatwa nusu. Sasa sidhani kama mzigo huo ukikulalia, unaweza kutoka hapo! Ni rahisi sana kuuumia hata kupoteza maisha.

"Hivi ninavyoongea kuna jamaa zangu ambao wamenifundisha kazi wameshafariki dunia kutokana na ajali za pikipiki na ambao tulikuwa kundi moja la watu 40, madereva sita wameshapoteza uhai kwa ajali ya kuangukiwa na mzigo.

Mwishoni mwa mwaka juzi na mwaka jana," Seif anasimulia madhila aliyopitia, akitaja muda wa safari zao ilikuwa kati ya saa saba hadi saa nane usiku, wakiamini hakuna askari wa TFS porini na barabarani.

SHERIA

Katika hilo, Seif na wenzake wanakiuka sheria za nchi. Sera ya Misitu ya Mwaka 1998 na Sheria ya Misitu Sura 323 (marejeo ya mwaka 2002).

Sheria hizo zinazuia shughuli za uzalishaji mkaa bila kibali na adhabu yake inaambatana na kutaifishwa chombo kinachotumika kusafirisha mazao ya misitu.

HALI ILIVYO

Kijana Seif anabainisha kuwa ndani ya mapori ya TFS katika eneo hilo la Mkoa wa Pwani, kuna vijana wanaofanya kazi ya aina yake zaidi ya 3,000 wanaoangamiza misitu kuwa mkaa, wakiishi katika hali ya kinyemela ambayo ni mtihani kwa askari wa TFS kuwabaini.

Anasimulia wakiwa wamejiunda katika staili ya makundi, wanatumia silaha za fimbo za jadi kukabiliana na TFS wanapotokea kutaka kuwadhibiti na mara nyingi wamekuwa wakiwazidi, hata ikawa chanzo cha askari hao wa serikali kutumia silaha za moto na zana za kisasa kwenye vita hivyo.

"Ukisikia TFS wanawasaka madereva wa mkaa, wewe utakavyotoka porini huangalii usalama wako, unachoangalia ni mzigo uliobeba, kwa sababu ukikamatwa pikipiki yako inachukuliwa na mzigo unachukuliwa.

Kwa hiyo, unakuwa hakuna kitu umefanya. Sasa ili kuepuka hayo yote, unabidi ukimbie hapo ndio ajali hutokea," anasimulia Seif huku huku akisisitiza mali aliyobeba ndio mtaji na tafsiri kuu ya maisha yake.

Seif anasema wanapokuwa na wenzake porini kusaka mkaa, anakiri wanakuwa na roho ya kikatili, yenye kumwona yeyote kikwazo kwao, wanaweza kumtoa uhai wake.

Anaeleza yalivyo mapambano yao barabarani, askari wa TFS huwasubiri kwa kuwavizia na kuna wakati wanachukua hata zaidi ya wiki porini pale wanapopata taarifa za nyendo za wabebaji mkaa ambao safari zao zinakuwa na pikipiki zinazofika 200.

Inapotokea mwendeshaji aliyedhurika vibaya au kupoteza maisha, Seif anadai askari wa TFS humwacha mhusika na kuchukua mali zake - pikipiki na mkaa, akitumia mfano wa madai ya kuwapo mkasa wa namna hiyo hivi karibuni eneo jirani na Mto Mondo, Kwala mkoani Pwani.

Anasema katika safari hizo, uhusiano wao na vijana wapelelezi wao, huwa wanachanga fedha kuwalipa kiasi cha Sh. 5,000 kwa kila mmoja kuwafanyia kazi hiyo, Seif akiainisha mbinu za wapelelezi wao:

"Hawa vijana kazi yao ni kuwafuatilia TFS, wakitoa gari tu, wanatupa taarifa na sisi tunaanza kujihami, maana wao wana mtandao mpana wa kujua kila kitu kinachofanywa na TFS dhidi yetu,

"TFS kwa sasa wanapokwenda porini wanafumua matanuri ya kuchomea mkaa," anasimulia Seif na kubainisha mbinu za mapambano hayo ya vikosi vya kiserikali katika kutetea uhai wa misitu.

Soko la Mkaa Mbezi Kwamsuguli biashara ikiendelea. Picha:Frank Monyo
MAUZO YA MKAA SOKONI

Seif anatanguliza hoja kwamba bidhaa hiyo ina soko kubwa. Namna wanavyoipata porini, wananunua mkaa kwa bei ya jumla Sh. 120,000 kwa gunia tatu na wanayauza kwa Sh. 320,000 rejareja.

"Wateja ni wengi sana, wanasimama barabarani wanatusimamisha, lakini soko kuu la mkaa ambalo bodaboda wote wanauza ni Mbezi kwa Njemba njia ya kwenda Goba, Mbezi kwa Yusuph.

Sehemu nyingine ni Kibanda cha Mkaa na (Mbezi), sehemu nyingine ni kuuzia mtaani, maeneo ya Kifuru, Maramba Mawili, hadi Gongo la Mboto," anakutaja kote mkoani Dar es Salaam.

Seif anadokeza siri ya pikipiki zao kuwa na uwezo wa ziada katika kubeba mzigo wa mkaa, kwamba zinafanyiwa marekebisho ya kiufundi, 'shokapu' zake zinaboreshwa kwa kuinuliwa, vilevile eneo la nyumba kunakobebwa mzigo.

Pia anaeleza vipindi linganifu vya kisheria dhidi ya biashara ya mkaa, akifafanua kuwa kuna wakati serikali ilikuwa imetoa rukhsa kwa bishaara ya mkaa, watu walikuwa wanalipa ushuru na anakiri kwa kutumia tathmini yake kwamba "ajali zilipungua" kwa kundi lao.

Anapofananisha ushuhuda binafsi wa mazingira, alipotakiwa kutoa tathmini yake, Seif anakiri hali ni mbaya, misitu inatoweka kwa kasi, akitumia mfano wa miaka mitatu pekee - eneo la Ruvu, misitu inatoweka kwa kasi kutokana na uchomaji mkaa.

Pia anataja Kitongoji cha Kwala anakoishi, kuelekea umbali wa kilomita 15 ambako kuna pori, nalo uchomaji mkaa ni hali mbaya.

Baadhi ya wachuuzi na wanunuzi wa Mkaa katika Soko la Mkaa Mbezi Kwamsuguli biashara ikiendelea. Picha:Frank Monyo

Itaendelea Kesho....