PURA yatakiwa kujipanga tukio la kutangaza vitalu vya mafuta, gesi asilia

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 07:46 PM Oct 22 2024
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati (anayeshughulikia masuala ya mafuta na gesi), Dk. James Mataragio akieleza jambo wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Pili wa Bazara la Pili la Wafanyakazi PURA uliofanyika  Jijini Tanga jana.
Picha:Mpigapicha Wetu
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati (anayeshughulikia masuala ya mafuta na gesi), Dk. James Mataragio akieleza jambo wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Pili wa Bazara la Pili la Wafanyakazi PURA uliofanyika Jijini Tanga jana.

NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Nishati (anayeshughulikia masuala ya mafuta na gesi), Dk.James Mataragio ametoa rai kwa Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) kujipanga vyema kufanikisha kazi ya kutangaza duru ya tano ya kunadi vitalu vya utafutaji wa mafuta na gesi nchini.

Dk. Mataragio alitoa rai hiyo jana jijini Tanga wakati wa ufunguzi wa kikao cha pili cha mkutano wa pili wa Baraza la Wafanyakazi PURA.

Katika hotuba yake ya ufunguzi, Dk. Mataragio aliitaka PURA kuhakikisha kuwa inajitoa kwa hali na mali kufanikisha kazi hiyo muhimu kwa nchi ili kuvutia uwekezaji katika shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia nchini.

"PURA mna kazi kubwa kama taasisi kuhakikisha kwamba hii 'licensing round' inafanyika vizuri na tunapata matokeo mazuri" alisema Dk.Mataragio. 

Tukio la kutangaza duru ya tano ya kunadi vitalu vya utafutaji wa mafuta na gesi asilia nchini linatarajiwa kufanyika Machi mwaka kesho katika Kongamano na Maonesho ya Mafuta na Gesi Asilia kwa Afrika Mashariki litakalofanyika Jijini Dar es Salaam. 

Kongamano hilo linaloandaliwa na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki linatarajiwa kuleta pamoja wadau zaidi ya 1000 kutoka ndani na nje ya Afrika Mashariki kwa lengo la kujadili uendelezaji endelevu wa rasilimali za mafuta na gesi asilia zilizopo katika nchi wanachama.