Asisitiza miradi taka sifuri ifike mitaani

By Jenifer Gilla , Nipashe
Published at 05:11 PM Oct 22 2024
Mkuu wa Kitengo cha Uhifadhi wa Taka na Usafi wa Mazingira cha  jiji la Dar es Salaam, Philipo Beno.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkuu wa Kitengo cha Uhifadhi wa Taka na Usafi wa Mazingira cha jiji la Dar es Salaam, Philipo Beno.

TAASISI zinazotekelesa miradi ya taka sifuri zimesisitizwa kupeleka miradi hiyo katika ngazi ya mitaa, ili kupunguza idadi ya taka zinazopelekwa dampo ambazo nyingi hutupwa ovyo mitaani.

Mkuu wa Kitengo cha Uhifadhi wa Taka na Usafi wa Mazingira cha  jiji la Dar es Salaam, Philipo Beno, aliyasema hayo mwishoni mwa wiki  wakati alizindua mradi wa taka sifuri katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Jangwani unaosimamiwa na Shirika la Mazingira Plus.

Alisema kwa sasa jiji la Dar es Salaam tani 1320 kwa siku, kati ya hizo ni asilimia 6.5 tu ndio zinarejeshwa, hivyo kuwa na idadi kubwa ya taka zinazopelekwa dampo na nyingine hutupwa ovyo mitaani. 
Aidha, alisema miradi hiyo ikipelekwa kwa wananchi wa kawaida katika ngazi ya mitaa itakuwa msaada mkubwa wadhibiti taka nyingi kupelekwa kwente madampo ambayo nayo yamesidiwa na wingi wa taka. 

"Halmashauri ya jiji la Ilala kwa siku wanazalisha tani 1,320 za taka hiyo ni kwa siku, taka hizi zote zinatakiwa zitolewe na  kupelekwa dampo,tukikaa vizuri na taka sifuri suala hili likashuka chini kwa jamii  tukafanya utaratibu wakutenganisha taka ambapo kufanya hivyo dampo litachukua taka chache,"alisema Beno. 

Alisema halmashauri ya Ilala  imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutenganisha taka hatarishi za hospitalini hivyo nguvu kama hiyo pia inahitajika katika utenganishwaji wa taka za nyumbani.

Alisema mradi wa taka sifuri shuleni utasaidia kwa  kikubwa kwa wanafunzi na walimu kwa kuwa elimu hiyo wataipeleka katika jamii na kuanza kutenganisha taka. 

"Mradi huu wa taka sifuri shuleni unasaidia kutengeneza jamii ya vijana itakayoleta mapinduzi katika utunzaji wa taka, pia kupitia taka hizi tutafadika kwakupata mbolea mbalimbali,"alisema Beno. 

Naye Mkuu wa Kitengo cha Mazingira katika Taasisi ya Mazingira Plus, Ramadhani Mwakae alisema shule hiyo ni ya pili kukabidhiwa mradi wa taka sifuri na kuitaja shule ya kwanza kuikabidhi ni  ya Shule ya Sekondari Kibasila  iliyopo Wilaya ya Temeke. 

Alisema watakabidhi  mradi  kama huo katika Shule ya Sekondari ya Dar es Salaam iliyopo wilaya ya Ilala na matarajio yao ni kukabidhi miradi hiyo kwa shule zote za sekondari na msingi nchini.

"Dhumuni la mradi huu ni kupambana na mabadiliko ya tabia nchi hususani kudhibiti  uchafuzi wa taka mashuleni lakini,pia malengo ya mradi huu ni kufanya uchechemuzi wa sera na kuishauri serikali kusimamia utekelezaji wa sera, ”alisema. 

Alisema takwimu zinaonyesha tatizo mabadiliko ya tabia nchi ni tatizo la kimazingira hasa plastiki na taka ozo na kuyasihi mashirika yasiyokuwa na serikali yaongane nao katika kampeni hiyo  ili ifikapo  2030 jamii itengeneze mtandao wa taka sifuri. 

Mwakilishi wa Taasisi ya Kimataifa ya Nagu, iliyofadhili mradi huo, Dorothee Braun aliipongeza Mazingira Plus kwa kubuni mradi huo utakaoleta mabadiliko makubwa katika uhifadhi wa mazingira.  

"Katika miradi hii shule moja inagharimu Euro 5,000 (Sh.milioni 14.8) mpaka 7,000 (Sh.milioni 20.7)  sisi tunataka waendelee katika shule zote ikiwamo za vijijini,” alisema Dorothee.