Rais Samia, Nyusi wakubaliana kuinua biashara iliyoporomoka

By Gwamaka Alipipi , Nipashe
Published at 09:01 AM Jul 03 2024
Rais Samia Suluhu Hassan akiwa na mgeni wake, Rais wa Msumbiji, Filipe Jacinto Nyusi baada ya kuwasili katika viwanja vya Ikulu, jijini Dar es Salaam jana.

RAIS Samia Suluhu Hassan na mgeni wake, Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi, wamesema biashara na uwekezaji kati ya nchi hizo mbili zimeshuka na kunahitajika ufufuaji wa haraka.

"Mwaka 2022 kiwango cha ufanyaji biashara kati ya Tanzania na Msumbiji kilikuwa Dola za Marekani milioni 57.8 lakini mwaka jana kilishuka hadi Dola za Marekani milioni 20.1," alitamka Rais Samia jana Ikulu jijini Dar es Salaam. 

"Kwahiyo, tukaangalia nini kimesababisha anguko hilo. Tukakubaliana kushirikiana ili kuongeza," Rais Samia aliongeza wakati wakuu hao walipozungumza na waandishi wa habari baada ya mazungumzo yao ya faragha. 

Rais alitaja maeneo 10 waliyokubaliana kushirikiana kiuchumi, yanajumuisha biashara, uwekezaji, sekta ya nishati, uchumi wa bluu, kilimo, ulinzi na usalama, sekta ya afya, miundombinu, ujenzi wa kituo cha forodha pamoja na kujumuisha ushirikiano huo na Afrika. 

Rais Samia alisisitiza hali ya uwekezaji kati ya nchi hizo jirani si nzuri na ndiyo imejenga azma ya kuundwa ushirikiano huo, akitoa mfano, nchini kuna wawekezaji wawili tu kutoka Msumbiji huku Watanzania 16 ndiyo wamewekeza Msumbiji. 

"Namba hii ni ndogo, imetushtua hata sisi. Hivyo, tumekubaliana kuongeza. Katika wawekezaji hao wa Msumbiji waliopo hapa Tanzania wameleta ajira 650," alisema Rais Samia, huku akitaja mahususi wamekubaliana kuendeleza vyanzo vya nishati ya umeme kwa pamoja. 

Alitaja eneo lingine ni kwenye uchumi wa bluu, hususani sekta ya gesi, akibainisha Msumbiji ina akiba ya gesi yenye ujazo metriki trilioni 100, huku Tanzania ikiwa na ujazo wa metriki trilioni 57. 

Katika suala la masoko, Rais Samia alisema Tanzania na Msumbiji ni wazalishaji wa zao la korosho, lakini mamlaka ya upangaji bei zake iko katika soko la dunia. 

Hivyo, akadokeza kuhusu mkakati wao wa kuvunja ngome ya upangaji bei ni kupitia azma yao ya kuunda umoja wa wazalishaji korosho Afrika utakaokuwa na sauti ya kuamua bei katika soko hilo. 

Rais alisema wamekubaliana kushirikiana katika kuimarisha ulinzi na usalama mipakani, hususani kukomesha matukio ya kiharamia. 

Hiyo inakwenda sambamba na kuboresha afya kwa wananchi wao, huku mwenza wake mkutanoni, Rais Nyusi, mwenyeji nchini na mweledi wa Kiswahili, akifafanua: 

"Nchi zetu zinapakana, hivyo tunapaswa kukuza uchumi. Kunapaswa kuwapo utafiti wa korosho, ili (zao) liweze kunufaisha zaidi mataifa yetu." 

Alihitimisha hoja yake, akigusia namna walivyonufaika katika mazungumzo yao, yakigusa mengi ya kimaendeleo baina yao, kwa upekee akigusa eneo alilolipa umuhimu, uimarishaji miundombinu.