Nipashe namba moja uandishi habari za jinsia, jumuishi

By Grace Mwakalinga , Nipashe
Published at 10:54 AM Jul 03 2024
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communication Ltd, Bakari Machumu, akifungua mafunzo kwa waandishi wa habari na wakufunzi wa masuala ya jinsia na mawasiliano ( hawapo pichani) jijini Dar es salaam yanayoendeshwa na Chuo Kikuu cha Agha Khan.
PICHA: GRACE MWAKALINGA
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communication Ltd, Bakari Machumu, akifungua mafunzo kwa waandishi wa habari na wakufunzi wa masuala ya jinsia na mawasiliano ( hawapo pichani) jijini Dar es salaam yanayoendeshwa na Chuo Kikuu cha Agha Khan.

GAZETI Nipashe limeshika nafasi ya kwanza nchini kwa weledi wa kuandika habari zinazohusu masuala ya wanawake huku likiwa namba tano katika ukanda wa nchi za Afrika Mashariki.

Taarifa hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd, Bakari Machumu wakati akifungua mafunzo kwa waandishi wa habari na wakufunzi wa masuala ya jinsia na mawasiliano yaliyoandaliwa na Chuo Kikuu cha Agha Khan Graduate School of Media and Communications

Alisema matokeo hayo yametolewa kutokana na ripoti ya ‘State of Media reporting in East Africa’ kwa kuhusisha vyombo mbalimbali vya habari ukanda wa Afrika Mashariki.

Alisema ripoti hiyo inafafanua kuwa gazeti la Nipashe limeandika mada 225 zinazohusu masuala ya wanawake na kufikisha asilimia 20, huku gazeti la Daily Nation la nchini Kenya likiandika mada 306 na kufikisha asilimia 24.

“Gazeti la Nipashe ndilo namba moja hapa nchini kwa kuandika habari zinazohusu masuala ya wanawake kwa asilimia 20 likifuatiwa na Mwananchi ambalo limeandika kwa asilimia tisa, tunawapongeza kwa jitihada hizo naamini na vyombo vingine vya habari vitaendelea kuandika ili kuwapa nafasi wanawake,” alisema Machumu.

Kwa mujibu wa Machumu, Nipashe pia linafanya vizuri kidijitali kuandika habari za wanawake kwa ukanda wa Afrika Mashariki na limekuwa namba nne huku likiwa nafasi ya kwanza Tanzania likipiku vyombo vingine vya kidijitali.  

Alifafanua kuwa habari za wanawake zinazoandikwa zaidi zinahusu matukio, zikifuatiwa na masuala ya siasa, uchumi, biashara, utamaduni na dini.

“Maswala ya kijinsia sio masuala ya wanawake pekee. Napenda kusema kuwa kuripoti na kuwa na uwiano kuhusu masuala ya kijinsia ni vizuri kwa biashara kwenye vyombo vyetu vya habari nchini.”

Mkuu wa Chuo Kikuu cha Agha Khan kitivo cha Shule ya Uzamili wa Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma, Prof. Nancy Booker, wakati akizindua ripoti hiyo alisema kuwa katika utafiti huo gazeti la Nipashe limekuwa kinara kwa kuzingatia masuala ya jinsia zote katika uandishi wake.

Utafiti huo ulifanywa mwaka 2023 Juni hadi Desemba kwa kuhusisha vyombo vikubwa vya habari katika nchi za Afrika Mashariki 19 na Nipashe kuibuka kinara katika kuandika masuala ya wanawake na kuzingatia usawa wa jinsia.

“Katika uandishi wake Nipashe iliweza kuzingatia masuala ya wanawake na imefanya jitihada wanawake kujulikana na sauti zao kusikika zaidi,” alisema Prof. Nancy.

Prof. Nancy alitoa wito kwa vyombo vingine vya habari nchini kuiga mfano wa Nipashe kwa kuwa kwa sasa dunia nzima haina masuala ya jinsia na kuvitaka kuandika kwa kuzingatia usawa.

“Masuala ya jinsia yamekuwa mtambuka ulimwenguni mabadiliko ya sayansi na teknolojia yamechangia kuongeza ujuzi wa mambo, hivyo ni vyema vyombo vya habari kuandika habari kwa kuhusisha vyanzo mbalimbali vya habari ili kutoa nafasi kwa jinsia zote na kusaidia kundi la wanawake kufanya maamuzi ndani ya vyombo vya habari,” aliongeza Prof. Nancy.