Mgombea wa nafasi ya Umakamu Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAWACHA), Moza Ally, amesema endapo atashinda nafasi hiyo, atajitahidi kuwainua wanawake kiuchumi na kuwahamasisha kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.
Moza alitoa kauli hiyo leo, Januari 5, jijini Dar es Salaam, alipokuwa akiambatana na wenzake kurejesha fomu za kuwania nafasi mbalimbali katika ofisi ndogo za chama hicho zilizopo Kinondoni.
Wengine waliorejesha fomu ni Michael Materu, anayewania nafasi ya Mweka Hazina wa Baraza la Vijana CHADEMA (BAVICHA), Masud Mambo anayegombea Uenyekiti wa baraza hilo Taifa, na Revline Mbugi anayewania Unaibu Katibu Bara wa BAVICHA.
Moza amesema ameamua kugombea nafasi hiyo ya BAWACHA kwa sababu amebaini kuwepo kwa pengo kubwa katika juhudi za kuwahamasisha wanawake kushiriki siasa kikamilifu.
"Uimara wangu hauna shaka. Kama mnakumbuka, juzi nikiwa mkoani Mbeya niliweka wazi dhamira yangu na kusimama imara kama mwanachama wa BAVICHA. Sasa nipo tayari kuimarisha BAWACHA kwa kushirikiana na kuhamasisha wanawake waliopo ndani na nje ya chama," amesema Moza.
Aidha, ameongeza kuwa ni muhimu kuwajengea wanawake uwezo wa kugombea nafasi za juu za uongozi, akibainisha kuwa kwa sasa hakuna mwanamke hata mmoja anayegombea nafasi mbili za juu za uongozi wa chama hicho.
"Tunajukumu la kuhakikisha wanawake wanajiamini na kugombea nafasi za juu. Ikiwa nitashinda, katika chaguzi zijazo nitalenga kugombea nafasi za Mwenyekiti Taifa na Makamu Mwenyekiti," alisisitiza Moza, ambaye kabla ya kutia nia katika nafasi hiyo alikuwa Makamu Mwenyekiti wa BAVICHA.
Kwa upande wake, Mgombea wa Uenyekiti wa BAVICHA Taifa, Masud Mambo, amesema atajikita kudai katiba mpya na tume huru ya uchaguzi endapo atachaguliwa.
"Nitahakikisha tunapanga mikakati itakayosaidia BAVICHA kuinua vipaji kwa vijana na kuwahamasisha kushiriki katika siasa na kugombea nafasi za uongozi," amesema Masud.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED