Mbunge kuiomba serikali kutenga siku kwa makundi ya WhatsApp

By Thobias Mwanakatwe , Nipashe
Published at 08:39 AM Jan 01 2025
MBUNGE wa Iramba Mashariki, Francis Mtinga
Picha:Mtandao
MBUNGE wa Iramba Mashariki, Francis Mtinga

MBUNGE wa Iramba Mashariki, Francis Mtinga amesema atawasilisha hoja binafsi bungeni kuiomba serikali iweke siku maalum ya makundi ya wanachama wa mitandao ya kijamii ya WhatsApp kufanya mambo yao na shughuli za maendeleo kwa jamii.

Mtinga alitangaza mpango wake huo juzi kwa wanafunzi waliosoma Shule ya Sekondari Mwenge iliyopo Manispaa ya Singida ambao wapo katika kundi moja la whatsApp kutoka mikoa mbalimbali nchini baada ya kukutana na kufanya kazi ya kupanda miti katika shule hiyo. 

Mtinga, alisema makundi hayo ya whatsApp yanawakusanya watu mbalimbali na baadhi yamekuwa na manufaa makubwa kwa jamii kutokana na kushiriki shughuli mbalimbali za maendeleo na kusaidiana. 

Alisema hivyo kuna umuhimu wa kutenga siku maalum itambulike kisheria kwa ajili ya shughuli hiyo. 

Alisema suala hilo ambalo anaamini ataungwa mkono na wabunge wenzake, makundi ya whatsapp yatakapokuwa yametambulika rasmi kisheria hata taasisi, mashirika na kampuni yatakuwa yanawaruhusu wafanyakazi wao kwenda kushiriki shughuli itakayokuwa imeandaliwa na kundi lao. 

"Baadhi ya wanachama wa makundi ya mitandao ya kijamii ya WhatsApp wanapokuwa wana jambo lao la kwenda kufanya nje, mfano ya kituo cha kazi inakuwa vigumu kwenda kwa bosi wake kuomba ruhusa kwasababu suala la group la whatsApp halitambuliki," alisema. 

Mtinga aliwaomba wabunge wenzake siku atakapowasilisha hoja bungeni aungwe mkono ili serikali ikubali kutenga siku maalum ya makundi hayo. 

Makundi ya mitandao ya kijamii ya WhatsApp huwa yanawasilisha umoja wa watu kuwa na malengo yanayofanana. 

Mfano makundi ya shule na vyuo  huwa hayana dhamira ya kutaka kusalimiana na kujuliana hali, bali  yapo pale maalum kupima mafanikio ya walio kwenye kundi.