Mbaroni tuhuma kuua msichana wa kazi

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 06:05 AM Aug 25 2024
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Wilbrod Mutafungwa.
Picha: Mtandao
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Wilbrod Mutafungwa.

JACKSON Magoti (30), mkazi wa Michese Tanesco, jijini Dodoma, anashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Mwanza kwa tuhuma za mauaji ya mfanyakazi wa ndani, Sainethi Kakululu (20), mkazi wa Mtaa wa Ipuli, Mahina, jijini hapa.

Taarifa ya kukamatwa kwa Magoti ilitolewa jana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Wilbrod Mutafungwa wakati anazungumza na waandishi wa habari. 

Kamanda Mutafungwa alisema mtuhumiwa huyo alitiwa mbaroni Agosti 16 mwaka huu, saa 5:30 asubuhi jijini Dodoma alikodaiwa kukimbilia baada ya kutekeleza mauaji hayo. 

"Mtuhumiwa huyu alikuwa anafanya kazi ya kusafisha bustani ya nyumba ya Jackline Ngowi, ambako pia alikuwa anafanya kazi za ndani Sainethi.  

"Uchunguzi wa awali umebaini alitekeleza mauaji hayo ili kutimiza azma ya kuiba mali zilizokuwa ndani ya nyumba ya Ngowi," alidai Kamanda Mutafungwa. 

Alisema Magoti anadaiwa kumuua msichana huyo kwa kumkaba shingoni, kisha kupora vitu mbalimbali ndani ya nyumba hiyo alimokuwa anafanyia kazi. 

Alisema kuwa baada ya mauaji hayo, Agosti 5 mwaka huu, saa 11:30 jioni, Jeshi la Polisi lilianza kumfuatilia mtuhumiwa na ndipo alipokutwa nyumbani kwao Dodoma. 

"Alikutwa na vielelezo mbalimbali alivyopora ikiwamo simu ya marehemu, viatu pamoja na baadhi ya nguo za marehemu," alisema. 

Kutokana na tukio hilo, Kamanda Mutafungwa aliwataka wananchi kutoa taarifa za wahalifu na uhalifu haraka pindi wanapoubaini ili kusaidia jeshi hilo kuchukua hatua za haraka. 

Alisema Jeshi la Polisi linaendelea na operesheni katika maeneo ya Ziwa Victoria ili kudhibiti wahalifu na uhalifu ziwani huko. 

Kwa mujibu wa Sheria ya Kanuni za Adhabu, Sura ya 16, adhabu ya kuua kwa kukusudia ni kunyongwa hadi kufa, hivyo kijana huyo akithibitika mahakamani kufanya mauaji hayo, atakabiliwa na adhabu hiyo.