Mfumo wa kuunganisha watoa huduma kifedha waandaliwa

By Faustine Feliciane , Nipashe
Published at 12:44 PM Sep 13 2024
Naibu Gavana  wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Sauda Msemo
Picha:Mtandao
Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Sauda Msemo

SERIKALI imesema imeandaa utaratibu utakaowezesha ushirikiano kati ya benki na watoa huduma za fedha kwa njia ya mtandao ili kuimarisha huduma hiyo nchini.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam kwenye Kongamano la Wafanyabisahara na wawekezaji Afrika Mashariki, Naibu Gavana  wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Sauda Msemo, alisema kwa sasa teknolojia inazidi kukua, hivyo ni muhimu kwenda nayo sambamba. 

"Huduma hizi za kifedha kwa njia ya mtandao zinazidi kukua na serikali tayari imeandaa utaratibu mzuri kwa pande hizi mbili kushirikiana ili kusaidia kukuza huduma hii," alisema Msemo. 

Katibu Mtendaji wa Chama cha Watoa Huduma za Kifedha kwa Njia ya Mtandao (TAFINA), Shedrack Kamenya, alisema malengo makubwa ya kuwakutanisha watoa huduma za kifedha na watunga sera na wadau wengine ni kuangalia namna ya kukuza sekta hiyo pamoja na kuangalia changamoto za wizi wa fedha katika huduma hizo.

"Moto wetu mkubwa ni kuwekeza na kuingia ubia kuhakikisha watu wote wanaingia katika utoaji huduma za kifedha kwa mtandao, lakini pia maeneo tunayoyaangazia ni mazingira ya kifedha kusaidia upatikanaji wa huduma na wizi wa fedha kwa njia ya mtandao," alisema Kamenya. 

Pia alisema wizi wa fedha kwa njia ya mtandao ni eneo muhimu ambalo wanaliangazia katika kongamano hilo ili kupata njia ya kudhibiti. Alisema  kampuni 10 kutoka nchi mbalimbali zinashiriki katika kongamano hilo la siku mbili.

Mmoja wa washiriki wa kongamano hilo, ambaye ni Meneja wa Soko la Afrika wa kampuni ya G-Payment, Alfred Tembo, alisema TAFINA imeona umuhimu wa kushirikisha nchi za Afrika Mashariki katika kukuza sekta hiyo nchini.

"Lakini pia nipongeze utayari wa serikali ya Tanzania katika kupokea wawekezaji hasa kwenye sekta hii ili kurahisisha ulipaji fedha katika huduma mbalimbali," alisema Tembo.