Maajabu ya kaburi la Chifu wa Wangoni yanavyowavutia watalii wa kiutamaduni

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 05:03 PM Sep 17 2024
Wakina mama wakifanya dua zao kama sehemu ya mila za Kingoni kwenye kaburi la Chifu Ngosi Mharule.

KUELEKEA Tamasha la Kitaifa la Utamaduni, linaloanza Septemba 20 hadi 23 mwaka huu, wakazi wa kijiji cha Mbingamharule wilaya ya Songea mkoani Ruvuma wanaelezea vivutio vilivyopo mkoani humo ikiwamo kaburi lenye maajabu la kiongozi wao kimila, Chifu Ngosi Mharule bin Zulu Gama.

Agnes Ngonyani ni msimamizi wa kaburi hilo la kihistoria kwa sasa. Kaburi hilo lililojengewa kwa umbo la duara kwenye eneo la heka nane ni moja ya vivutio vya utalii wa kiutamaduni vinavyopatikana katika kijiji hicho cha Mbingamharule, Songea mkaoni Ruvuma. 

Chifu Mharule alitokea nchini Afrika Kusini na kwenda kutawala katika kabila hilo la Wangoni kuanzia mwaka 1847 hadi 1889 alipofariki na kuzikwa  kijijini hapo. 

Historia inaonyesha kuwa baada ya kufariki Chifu Mharule, alizikwa kwa kufuata desturi na mila za kichifu za kabila la Wangoni toka Afrika Kusini na wakati anazikwa, walichukuliwa watu wengine wawili wakiwa hai na kuzikwa naye kwenye kaburi moja. 

“Chifu Mharule baada ya kufariki mwaka 1889, alizikwa kwa taratibu za jadi ya machifu wa Afrika Kusini, kaburi lake lilikuwa la mviringo, sanda yake ilikuwa ya ngozi, alikarishwa kwenye kiti cha ngozi na walichukuliwa na watu wengine wawili wakiwa hai ambao walizikwa pamoja naye kwenye kaburi moja wakiwa wamesimama mbele na nyuma ya mwili wa Chifu,” anasema mmoja wa Wazee kijijii hapo, Christian Ngonyani. 

Anasema kwa historia ya mila na desturi ya Kingoni, taratibu za kijadi za wakati huo zilitaka mfalme au chifu anapofariki ni lazima azikwe na watu wawili wakiwa hai na kwamba hiyo ilikuwa ni amri ya serikali ya jadi na hapakuwapo na mtu aliyepinga.

Kwa mujibu wa mzee Ngonyani, wengi waliokuwa wakizikwa na mfalme wakiwa hai ni wale ambao walikuwa wamezoeana na kufanya kazi kwa karibu.

Mbali na shughuli za utalii, kaburi hilo limekuwa likitumiwa na wananchi wa maeneo hayo kwenda kuhiji kila mwaka na kwamba hata ndugu wa Chifu Mharule toka Afrika Kusini huwa wanafika kufanya matambiko kwenye kaburi hilo.

"Mwaka 2019 ukoo wa Chifu Mharule kutoka Afrika Kusini ulifika kushuhudia kusimikwa kwa Chifu Nkosi Imanuel Zulu Gama wa tano ambaye ndiye Chifu wa Wangoni kwa sasa. Kwa hiyo yeyote anayependa kwenda kutembelea kaburi hilo, kuna taratibu zake za kimila ambazo zinatakiwa kufuatwa ambazo ni kubeba mahindi na ulezi ambao unatengenezwa na bibi katika kijiji hich,”anasema Ngonyani.

"Baada ya kufika eneo la kaburi, anatangulia mhusika ambaye anawasiliana na Chifu kwa lugha ya jadi, ndipo waliofika kutambika wanaitwa na kupiga magoti juu ya kaburi na kuomboleza kwa kwa sala za jadi. 

 “Baada ya maombi kuku au mbuzi wanachinjwa juu ya kaburi la Chifu Mharule lakini jambo la kushangaza mbuzi huyo anapochinjwa hapigi kelele na baada ya kuchinjwa mmoja wa watambikaji anamwaga unga wote juu ya kaburi." 

Ngonyani, anasema jambo jingine la kushangaza ukienda kesho yake asubuhi kwenye kaburi hilo hauoni damu wala unga, vyote vinakuwa vimeliwa na kwamba hiyo ndiyo ishara ya kukubaliwa shida zote ambazo mhusika wa kutambika alikwenda nazo kuomba kwenye kaburi hilo. 

Agnes ambaye amepewa kazi ya kusimami kaburi hilo kwa sasa, anasema wamekuwa wakipokea wageni wengi wanaotembelea kaburi hilo na kwamba wapo ambao wanatoka mpaka nchi za Ulaya, Marekani na Afrika ambao nao huenda kuomba kutatuliwa shida zao mbalimbali, kuhiji na kufanya matambiko. 

Agnes anasema maajabu mengine yaliyopo katika kaburi hilo ni pamoja na kuwapo kwa nyoka ambaye huonekana baada ya miaka mitano au kumi ambaye hata hivyo anapojitokeza kwa kipindi hicho ni watu watu ambao hubahatika kumuona. 

“Huyu nyoka haonekani mara kwa mara isipokuwa baada ya miaka mitano au kumi tena akijitokeza, watu wachache sana ndio hubahatika kumuona na akionekana huwa anaenda bondeni kunywa maji,”anasema Agnes.

 Agnes anasimulia kwamba eneo hilo la kaburi linaheshimika na hakuna mtu mwenye udhubutu wa kufanya uharibifu wowote. 

“Kwa mfano kwenye kaburi hilo la Chifu Mharule, kuna mtu aliwahi kwenda akaezua paa lakini hakuchukua hata mwezi mmoja alifariki, kwa hiyo tunaamini kwamba sababu hiyo ndio ilisababisha kifo chake,”anasema Agnes.