Kaburi la mtoto lafukuliwa

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:13 AM Sep 19 2024
toto Faston Innocent likiwa limefukuliwa na watu wasiojulikana katika Kijiji cha Katunga, Kata ya Bugombola, wilay- ani Karagwe, mkoani Kagera jana.
PICHA: RESTUTA DAMIANI
toto Faston Innocent likiwa limefukuliwa na watu wasiojulikana katika Kijiji cha Katunga, Kata ya Bugombola, wilay- ani Karagwe, mkoani Kagera jana.

KATIKA hali isiyo ya kawaida, mwili wa mtoto Faston Innocent (1) umefukuliwa na watu wasiojulikana huko Kahinga, Kata ya Bugomola, wilayani Kyerwa, mkoani Kagera kisha jeneza lake kuwekwa kwenye mlango wa nyumba ya babu yake, Venant Zabron (52).

Akisimulia tukio hilo, babu wa mtoto huyo, Zabron, alisema lilitokea Septemba 17 mwaka huu na kuibua taharuki kwa familia hiyo pamoja na majirani.

Alisema kuwa wakati akiwa ndani ya nyumba yake, alisikia kelele za majirani waliokuwa wakipita kwake lakini hakubaini haraka kilichokuwa kinaendelea.

"Tulipotoka, tuliona jeneza likiwa limefunuliwa na ndani yake kukiwa na mwili wa marehemu mjukuu wangu ambaye tulimzika siku chache zilizopita huku vitu vingine kama mashuka na msalaba vikiwa katika eneo hilo," alisema Zabron.

Alisema kuwa majirani walishangaa huku familia yake nayo ikishtushwa na kitendo hicho kinachodaiwa kufanywa na watu ambao hawakujulikana kwa mara moja.

Zabron alisema kuwa familia hiyo haikuwa na mgogoro wowote ndani ya jamii wanamoishi na hata kifamilia, hata watendwe kiasi hicho.

Kutokana na tukio hilo, baba mzazi wa mtoto huyo anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa madai ya kuhusika na ufukuaji mwili wa mtoto huyo kwa kile kinachodaiwa kuwa ulizikwa katika eneo ambalo yeye hakuridhia.

Jeneza la mtoto huyo, likiwa limetelekezwa mlangoni nje ya nyumba ya Venant Zabron ambaye ni babu wa marehemu. PICHA: RESTUTA DAMIANI
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kyerwa, Turakira Twijuke, akizungumza na Nipashe jana, alisema kuwa usiku wa kuamkia jana, alipokea mgeni aliyeomba hifadhi huku akidai kutaka kwenda nje ya wilaya kwa ajili ya safari zake za kawaida.

Twijuke alisema kuwa kijana huyo alijitambulisha kwa jina mmoja tu la Innocent lakini baada ya kumhoji ilibainika kuna kitu amefanya na alihitaji kutoroka kwenda nje ili kukimbia suala hilo.

Alisema kuwa ilipofika asubuhi, alianza safari kumpeleka kituo cha polisi lakini baadaye alipokea taarifa za tukio hilo, hivyo kuamua kwenda naye katika eneo la tukio ambako alidai kuwa kijana huyo alizidi kuonesha wasiwasi, hivyo kushukiwa na wakalazimika kumpeleka kituo cha polisi kwa mahojiano zaidi.

"Alipohojiwa alikiri kuwa huyo mtoto ni mwanawe na alizikwa katika eneo ambalo yeye hakuridhia, hivyo akalazimika kutenda tukio hilo kwa lengo la kuishtua familia hiyo itambue kuwa baba wa mtoto hakupendezwa mwanawe kuzikwa katika eneo hilo," alidai Twijuke.

Alisema kuwa baada ya mahojiano hayo, aliachwa kituoni huko kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria na mahojiano zaidi juu ya tukio hilo lililozua taharuki kwa wakazi wa eneo hilo.

Nipashe ilimtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Bratius Chatanda, ili kuthibitisha tukio hilo na hatua za kisheria zilizochukuliwa lakini hakupatika na kwa kile kilichoelezwa kuwa alikuwa nje ya kituo cha kazi kwa shughuli maalum.

Mkuu wa Kituo cha Kata ya Murongo, Peter Lugenzi, alisema  tayari jeshi hilo limechukua hatua lakini yeye hawezi kuzungumzia suala hilo kwa kuwa msemaji ni Kamanda wa Polisi Mkoa.