Kigogo CHADEMA akamatwa kwa tuhuma za jinai

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:29 AM Sep 19 2024
 Boniface Jacob.
Picha: Mpigapicha Wetu
Boniface Jacob.

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema kada wake, Boniface Jacob amekamatwa na Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam.

Akizungumza na Nipashe jana, Mkurugenzi wa Itifaki na Mawasiliano ya Mambo ya Nje, John Mrema, alisema kuwa Jacob alikamatwa jana eneo la Sinza na watu waliovalia sare za polisi kisha kumpeleka Kituo cha Polisi Oysterbay.

"Ni kweli Jacob amekamatwa leo (jana) maeneo ya Sinza na watu waliojitambulisha kuwa ni polisi, hivi sasa tumewatuma mawakili wetu waende kufuatilia kubaini nini kosa na taratibu zingine," alisema Mrema.

 Alisema kuwa Boniface alikamatwa saa 11:09 jioni, polisi wawili wenye sare na watatu wasiokuwa na sare, wakiwa wamebeba silaha, walifika alikokuwa na kumkamata kwa nguvu na kuondoka naye.

Hata hivyo, kupitia mtandao wa X wa Mrema aliandika: “Polisi wa Osyterbay wanaelekea nyumbani kwa Boniface Jacob muda huu kwenda kufanya upekuzi. Hawajasema wanachokwenda kukipekua, Mawakili wetu wapo na wataambatana naye kuelekea kwenye upekuzi huo."

Taarifa za kukamatwa kwa Boniface ambaye aliwahi kuwa Meya wa Ubungo zilianza kusambaa katika mitandao ya kijamii jioni zikieleza kuwa alikamatwa na askari polisi waliovalia sare, wengine wakiwa wamevaa kiraia waliokuwa na 'defender'.

Jeshi la Polisi kupitia Msemaji wake, DCP David Misime lilithibitisha kumshikilia kigogo huyo wa CHADEMA.

Katika taarifa yake, DCP Misime alisema "Jeshi la Polisi limemkamata na linamshikilia Boniface Jacob, mkazi wa Mbezi kwa Msakuzi, jijini Dar es Salaam kutokana na makosa ya kijinai anayotuhumiwa nayo. Hivyo wananchi wapuuze uongo unaosambazwa mitandaoni kuwa ametekwa." 

Mei 6, mwaka huu Boniface, maarufu Boni Yai, alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu mashtaka matatu ya kuchapisha taarifa za uongo kinyume cha sheria. Pia ndiye aliyefichua tukio la ukatili dhidi ya 'Binti wa Yombo Dovya'.