Muhimbili yapokea vifaa vya upasuaji macho kwa tundu dogo

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 07:50 AM Sep 19 2024
Muhimbili yapokea vifaa vya  upasuaji macho kwa tundu dogo
Picha: MNH
Muhimbili yapokea vifaa vya upasuaji macho kwa tundu dogo

HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (MNH) imepokea mashine mbili za kisasa zilizogharimu Sh. 68,247,700 kwa ajili ya upasuaji wa macho kwa njia ya tundu dogo kwa wagonjwa wenye tatizo la mtoto wa jicho.

Vifaa hivyo (surgical consumable and medicine na phacoimuisifier) vimetolewa na Vision Care kupitia Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Korea (KOICA).

Bingwa wa Macho na Mkuu wa Idara ya Macho MNH, Dk. Joachim Kilemile, akizungumza jana jijini Dar es Salaam kuhusu kambi ya mafunzo ya siku tano na kupokea mashine hizo, alisema vifaa hivyo vitarahisisha matibabu, kuokoa muda na mgonjwa kupona mapema.

"Mashine hii ambayo kwa kifupi tunaita ‘phaco’ itafanya upasuaji kuwa rahisi si mara ya kwanza sisi kufanya upasuaji huu, ila kwa mashine hii itasaidia kufyonza ukungu katika la lenzi na kuweka lenzi nyingine mpya. Mtoto wa jicho maana yake ni lenzi ya jicho imeota ukungu.

"Mashine hii imeongeza ubora kwa sababu awali kwa mgonjwa mwenye mtoto wa jicho alitakiwa asubiri upasuaji hadi mtoto wa jicho akomae. 

"Sasa upasuaji hautasubiri hilo atafanyiwa mara tu atakapobainika, kwa gharama ya Sh. 300,000 kwa hospitali binafsi inafikia zaidi ya Sh. milioni mbili," alisema Dk. Kilemile.

Mwanzilishi na Mwenyekiti wa Vision Care duniani, Dk. Dong Hae Kim, alisema taasisi hiyo imeamua kushirikiana na MNH kwa kutoa mafunzo kwa wataalamu pamoja na kutoa vifaa.

Alisema mafunzo hayo ni pamoja na namna ya kutumia mashine hizo kwa matokeo bora ya matibabu, akisema ni hatua nzuri kwa kuwa vifaa hivyo vimekwishatumiwa kwa miongoni mwa madaktari bingwa wa macho.

Kaimu Mkurugenzi Huduma za Upasuaji MNH, akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji MNH, Dk. Ibrahim Nkoma, alisema upasuaji wa tundu dogo utafanyika kwa asilimia 60 hadi 70 na kwamba kati ya wagonjwa 10 wanaohudumiwa miongoni mwao sita watapatiwa huduma hiyo.

"Ninashukuru serikali yetu na Serikali ya Korea Kusini kupitia Vision Care na KOICA kwa kuimarisha huduma za kibingwa na bobezi MNH.

"Lengo ni kuwasogezea Watanzania huduma nchini badala ya kuzifuata nje ya nchi kwa gharama kubwa," alisema Dk. Nkoma.

Alisema MNH itawatumia wataalamu wake waliojengewa uwezo kuwapa mafunzo wenzao katika hospitali za kanda, rufani, mikoa na wilaya ili waweze kuwapatia huduma wagonjwa huko waliko.