Majaliwa azindua mfumo wa kielektroniki EPZA

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 12:36 PM Sep 13 2024
Majaliwa azindua mfumo wa kielektroniki EPZA
Picha:Mtandao
Majaliwa azindua mfumo wa kielektroniki EPZA

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amezindua rasmi mfumo wa Kielektroniki wa Kuhudumia Wawekezaji Kwenye Maeneo Maalum ya Kiuchumi na Mauzo ya Nje (EPZ), ili kutoa urahisi kwa wawekezaji popote walipo duniani kupata taarifa sahihi za uwekezaji nchini na namna ya kujisajili bila ya kufika nchini.

Mfumo huu ulioanzishwa na Mamlaka ya Kanda za Maendeleo ya Uwekezaji (EPZA) ni moja ya utekelezaji wa maagizo ya Raisi Samia Suluhu Hassan ya kutaka taasisi zinazosimamia uwekezaji kuendelea kutengeneza mazingira wezeshi ya kuvutia na kuendeleza uwekezaji nchini.

Uzinduzi huo ni moja ya tukio muhimu wakati wa hafla ya uzinduzi wa taarifa tano za Maboresho ya Mazingira ya Biashara na Uwekezaji na Nyenzo za Usimamizi wa Uwekezaji nchini uliofanyika Septembe 11, mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Waziri Mkuu aliagiza taasisi za serikali na mamlaka kuharakisha marekebisho ya sheria zitakazowezesha shughuli za biashara na kuhakikisha kwamba kanuni mpya zinaimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji.

“Masuala haya yanapaswa kuendana na kuweka kipaumbele katika kutoa huduma kwa haraka, kwa ufanisi, na kwa kufuata viwango vya kimataifa. Mamlaka zinapaswa kuwa na mifumo iliyo rahisi ya mawasiliano na wawekezaji na kuondoa vikwazo vilivyopo,” alisema.

Ripoti nyingine zilizozinduliwa ni pamoja na Mwongozo wa Kitaifa wa Maendeleo na Usimamizi wa Maeneo Maalum ya Kiuchumi (SEZ), Ripoti ya Tathmini ya Utekelezaji wa Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji; Ripoti ya Uwekezaji wa Kitaifa kwa mwaka 2023 na Mpango wa Mkakati wa Ofisi ya Rais, Mpango na Uwekezaji kwa kipindi cha 2024/2025 - 2025/2026.

Pia, aliziagiza taasisi za serikali na mamlaka kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi, kwa kuwa inaweza kutoa maarifa na mapendekezo muhimu kwa maboresho yanayohitajika.

Alisisitiza umuhimu wa mipango ya maendeleo kutoa mafunzo na huduma kwa wadau wa biashara, ikiwa ni pamoja na kuhamasisha matumizi ya zana mpya za usimamizi wa uwekezaji. 

Kupitia mfumo wa Kielektroniki wa Kuhudumia Wawekezaji Kwenye Maeneo Maalum ya Kiuchumi na Mauzo ya Nje (EPZ), wawekezaji watashughulikia masuala yao ya uwekezaji kwa haraka na ufanisi, bila kujali mahali walipo.

Mkurugenzi Mkuu wa EPZA, Charles Itembe, alisema kuwa uzinduzi wa mfumo huo mpya ni sehemu ya maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuweka mazingira bora ya biashara na uwekezaji nchini.

“Huduma hii muhimu inawakilisha hatua nyingine muhimu katika kuendeleza mazingira rafiki ya biashara nchini Tanzania,” alisema.

Alisema mfumo utarahisisha mchakato wa uwekezaji kwa kuondoa haja ya wateja kusafiri hadi ofisini kupata huduma.

Sasa wanaweza kujiandikisha mtandaoni, kupata leseni zao, na kupokea vivutio vinavyohitajika kutoka popote walipo.

Uzinduzi wa mfumo huo utaiwezesha Tanzania kushindana vema kuvutia uwekezaji wa kigeni mkubwa nchini.

Serikali inatazamia kuvutia uwekezaji wa ndani na wa kigeni, kuhamasisha ajira na kukuza maendeleo ya kiuchumi endelevu.