ACT Wazalendo yampa mtihani Rais Samia

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:40 AM Sep 13 2024
ACT Wazalendo yampa mtihani Rais Samia
Picha: Mpigapicha Wetu
ACT Wazalendo yampa mtihani Rais Samia

Chama cha ACT Wazalendo kimesema kuwa vitendo vya utekaji na mauaji ya watu wanaoikosoa Serikali kinatoa ishara kuwa Falsafa ya 4R ya Rais Samia Suluhu Hassan imezikwa rasmi.

Kurejesha imani, ACT Wazalendo imetoa changamoto kwa Rais Samia kuchukua hatua kwa vitendo ili kuonesha kuwa inatekeleza wajibu wake wa kulinda raia na mali zao na kujitenga na vitendo vya utekaji vinavyoendelea.

Akitoa changamoto hiyo kwenye Mkutano wa Hadhara katika Kijiji cha Mbawala, Jimbo la Mtwara Vijijini, Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu amesema ni lazima Waziri wa Mambo ya Ndani Hamad Masauni na IGP Wambura wawajibishwe kwa kuondolewa kwenye nafasi zao. Kuendelea kwao kuwa kwenye nafasi hizo, alisema Ado, kunaendelea kutoa picha kuwa Serikali ya Rais Samia inaunga mkono vitendo vya utekaji  na mauaji vinavyoendelea. 

Hatua ya pili, alisema Ado ni lazima jeshi la polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama vifanyiwe maboresho kwa kuzingatia mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai.

Mwisho, Katibu Mkuu Ado Shaibu amesema ni lazima mchakato wa Katiba Mpya uanze sasa ili kujenga msingi madhubuti wa kitaasisi katika kusimamia haki za watu. 

Katibu Mkuu Ado Shaibu anaendelea na ziara yake kwenye Mikoa ya Kusini na Kanda ya Ziwa. Leo anatarajiwa kuwa na ziara kwenye Jimbo la Mtama.