Askofu Mdegella aonya utekaji, mauaji

By Francis Godwin , Nipashe
Published at 11:03 AM Sep 13 2024
news
Picha: Mtandao
ASKOFU Mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Iringa, Prof. Owdenburg Mdegella.

ASKOFU Mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Iringa, Prof. Owdenburg Mdegella, amekemea matukio mauaji na utekaji yanayoendelea nchini na kuonya kuwa vitendo hivyo vinaweza kusababisha machafuko katika jamii.

Amesema Tanzania inapaswa kujifunza kutoka nchi zilizopitia katika hali hiyo ikiwamo jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) ambayo mpaka sasa hali ya amani ni tete. 

Prof. Mdegella, akizungumza na mwandishi wa habari hii ofisini kwake, mjini hapa, alisema matukio ya utekaji na mauaji9 yanayoibuka siku hadi siku nchini hali ambayo inatoa viashiria vya machafuko. 

Alisema  siku zote damu ya mwanadamu ina tabia ya kudai au kulia, hivyo kuendelea kwa matukio kikatili nchini, kutaliathiri taifa la Tanzania. Aliiomba serikali kuangalia namna ya kudhibiti matukio hayo ili kurudisha imani ya Watanzania kwa vyombo vya usalama.

"Yako mauaji ya aina nyingi. Mara  usikie watoto wameuawa, mara usikie watoto wamepotea na wamepatikana hawana viungo, mara viongozi fulani wa chama wanakufa kiajabu ajabu. Hapa  ninasema kama mtumishi wa Mungu. Nyie  mnaijua Congo ndiyo tajiri kwa nchi zote Afrika kwa maliasili, lakini haituli kutokana na damu ya Patrice Lumumba inalia," alisema. 

Askofu Prof. Mdegella alishauri viongozi wa juu wa nchi wajaribu kutumia mbinu kali  kuwawabana wanaosababisha vifo vya wengine bila sababu yoyote na vyama vya siasa kuachana na fitina za kisisa ili kukomesha mauaji.

Pia aliwataka wananchi wa mkoa wa Iringa kujitafakari upya ili kuona namna ya kuondokana na matukio mabaya yanayoonekana kushamiri zaidi ndani ya mkoa huo.

Alisema mkoa wa Iringa umekuwa na matukio ya kutisha kama vile ubakaji na ulawiti wa watoto, ulevi kupindukia, utapiamlo, kukithiri kwa imani za kishirikina na kuwa juu katika maambukizi ya Ukimwi jambo ambalo halileti taswira nzuri.

"Ninafikiria hata kuomba kibali cha serikali ili kupata nafasi ya kuzungumza mkoa kwa mkoa na hapa Iringa nitasemea Samora ili kukemea mambo haya ambayo yanatia kinyaa. Kila  siku tunasikia matukio ya kutisha na mengine yakifanywa na tuliotegemea watulinde. Damu  hii inayolia ikiendelea itatugusa hata tusiohusika," alisema.

Pia aliwakumbusha viongozi wanaoteuliwa kuwa na busara katika uzungumzaji wao ili kujiepusha na uzuaji wa taharuki kwa jamii wanayoiongoza.

"Mtumishi anayeteuliwa anapaswa kujua namna ya kutunza siri na ndiyo maana wanakula viapo," alisisitiza.

Katika hatua nyingine, Askofu Prof. Mdegella, alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan, kutokana na utendaji wake kuwa bora na kuongeza kuwa anajua kuna watu watamkosoa lakini kwa umri wake ameona marais wengi wa Afrika na utendaji wao, hivyo anavyompongeza na anatambua anachokisema.

"Mimi nimeangalia viongozi wengi wa Afrika lakini Rais Samia bado ni kiongozi mzuri.  Najua  watu wanasema anapewa pesa na Waarabu siju nini. Sasa  vitu kama hivi ulikuwa wapi wakati anapo pewa pesa hizo," alisema.