BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya Chalinze, Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani, limemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Ramadhani Possi kumuandikia barua Waziri wa Maji kukutana na Madiwani hao kutoa ufafanuzi kuhusiana na kero ya maji ambayo imekosa utatuzi.
Wamefikia hatua hiyo, baada ya maeneo mengi ya Halmashauri hiyo kuwa kero ya maji, huku jitihada za utatuzi zikigonga mwamba na kusababisha wananchi kutumia muda mwingi kutafuta maji.
Akizungumza kwenye kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika leo, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Hassan Kondo, amesema kutokana na kuwapo kwa kero ya maji katika maeneo mengi ni vema Waziri huyo afike na kutoa ufafanuzi.
Katika Baraza hilo, Madiwani wamelalamikia uongozi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dar es Salam (DAWASA) Chalinze, kutofanya kazi zao kama inavyotakiwa jambo linalosababisha wananchi kukosa maji.
Diwani wa Kimange, Ismail Msumi, ameeleza katika kikao hicho kwamba maeneo ya kata yake, siku 170 zimepita wananchi wa maeneo ya Kimange, Pongwe kuona na kikwazo kukosa maji.
Diwani wa Vigwaza, Mussa Gama, alisema miezi minne imepita bila kuwa na maji kwa wakazi wa kata hiyo, huku eneo la jirani Mlandizi maji yakipatikana bila kikwazo..
Gama ameeleza katika Baraza hilo kwamba, wananchi wake kwa sasa wanalazimika kununua dumu la maji lita 20 kwa Sh. 1,500 na kwamba pamoja na kufikisha taarifa hizo kwa mamlaka husika, bado hakuna hatua za utatuzi zilizochukuliwa.
Madiwani hao pia walihoji kuhusiana na Sh. milioni 500 zilizotolewa na Rais, kwa ajili ya kuunganisha maji kwa wananchi wa Chalinze, jambo ambalo halikupata majibu kama inavyotakiwa.
Akizungumza kwa niaba ya Meneja wa DAWASA Chalinze, Ofisa bBiashara DAWASA Chalinze, John Mmbaga, amesema tatizo lililopo katika kata ya Kimange, linaendelea kushughulikiwa na muda mfupi ujao maji yataanza kutoka.
Hata hivyo malalamiko mengine yaliyotolewa na madiwani hao, hayakupata majibu ikiwamo la Sh. mil. 500 za kusambaza maji, hali iliyowalazimu kuunga mkono hoja ya kumuita Waziri wa Maji, ambayo ilitolewa na Diwani wa Lugoba, Rehema Mwene.
Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Possi amesema anatarajia kutekeleza agizo hilo mapema, baada ya kupokea maagizo ya Baraza.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED