MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Shinyanga Mjini, Anord Makombe, amewaonya madereva wa bodaboda kuacha tabia ya kutongoza wake za watu pamoja wanafunzi.
Makombe amesema hayo wakati akizindua kituo cha maofisa usafirishaji bodaboda cha Majengo Mapya, sokoni, huku akiwasihi pia watii sheria za usalama barabarani.
Uzinduzi huo umefanyika jana, Februari 3, 2025 katika kituo hicho cha na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa CCM wilayani humo.
Makombe akizungumza wakati wa kuzindua kituo hicho, amewapongeza vijana hao kwa kujiajiri wenyewe na kuendesha maisha yao.
“Wakati wa usafirishaji muwe na maadili na kuacha kutongoza wake za watu, wakiwamo na wanafunzi kugeuza wake zenu, ili kituo hiki kiwe cha mfano kwa bodaboda wote.
“Kituo hiki cha bodaboda kimezinduliwa na CCM hivyo tunataka kiwe cha mfano kwa bodaboda wote, kuweni na maadili mema msivunje ndoa za watu,” amesema Makombe.
Aidha, akijibu maombi ya vijana hao juu ya mikopo ya pikipiki, amewaahidi kulishughulikiwa sababu ilani ya CCM inatamka juu ya kusaidia vijana, huku akiwasihi waendelee kujiunga kwenye vikundi vya vijana, ili wapate mikopo ya halmashauri asilimia 10 ambayo pia hutolewa kwa vijana.
Pia, amewasihi vijana hao waendelee kusomea mafunzo ya udereva kama ambavyo wanaendelea kufanya kwenye kikundi hicho, kwa kupeleka baadhi ya vijana kusomea udereva, ili wajue sheria za usalama barabarani na kwamba pia kuna fursa ya kusoma fursa mbalimbali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu.
Katika hatua nyingine, amewaomba wananchi waendelee kuiamini CCM, ili kiendelee kushika dola na kuendelea kuwaletea maendeleo pamoja na kutatua matatizo yao.
Katibu wa CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Hamisa Chacha, amepinga vikali baadhi ya watu ambao wamekuwa wakidharua kazi ya bodaboda na kubainisha kwamba kazi hiyo ni kama nyingine na ndiyo maana serikali ilitoa fursa ya kurahisisha usafirishaji.
Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Abdurazack Sakala, amesema vijana waendelee kuchangamkia fursa za mikopo ya halmashauri kupitia kwa maofisa maendeleo kwenye kata zao, ili kupata mikopo na kujikwamua kiuchumi.
Mjumbe wa kikundi hicho, Elias Kamuga,,akisoma taarifa, amesema kikundi chao kinazaidi ya miaka mitano na walianza wakiwa watu saba, lakini sasa hivi wamefikia 45 na wamepeleka baadhi ya vijana kusoma mafunzo ya udereva.
Amesema katika ya vijana hao 45 tayari wameshaunda kikundi cha watu watano, kwa ajili ya kuomba mkopo, huku wakiomba pia kusaidiwa kupata mikopo ya pikipiki.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED