KARIBU 2025... Samia: Tumevuna haya mwaka jana

By Jenifer Gilla , Nipashe
Published at 08:38 AM Jan 01 2025
Rais Samia Suluhu Hassan.
Picha: Mtandao
Rais Samia Suluhu Hassan.

RAIS Samia Suluhu Hassan ametaja mafanikio ya serikali yake kwa mwaka 2024, akijivunia kuvutia wawekezaji ambao miradi yao itazalisha ajira kwa watu 211,000 nchini.

Akihutubia kupitia vyombo vya habari vya Televisheni na Radio kufunga mwaka jana usiku, Rais Samia pia alisema ziara zake katika nchi 16 zimekuwa na tija kubwa, mojawapo ikiwa ni kuwezesha mafunzo ya urubani kufanyika nchini.

Katika ziara yake ya nchi ya Jamhuri ya Korea, akasema ilifanikisha kupatikana fedha zenye masharti nafuu Dola za Kimarekani bilioni 2.5 kwa ajili ya kutekeleza miradi katika sekta za maendeleo ikiwamo ujenzi wa kituo cha kisasa cha mafunzo ya reli.

Fedha hizo pia zitatumika kujenga chuo cha mafunzo ya anga na urubani, ujenzi wa kituo cha kusambaza umeme Nyakanazi, na kituo cha uchenjuaji wa madini na maabara za kisasa za vito, mradi wa uendelezaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kutoa ajira kwa vijana.

Alisema ziara hiyo pia ilifanikisha kusainiwa mkataba wa masharti nafuu wa  Dola za Marekani milioni 163.6 kwa ajili ya kugharamia mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Binguni na Kituo cha Mafunzo ya Afya huko Zanzibar.

Ziara ya nchini China ilifungua milango ya soko la bidhaa mbalimbali ikiwamo mihogo mikavu, soya, mabondo ya samaki, mazao ya baharini, asali, mashudu ya alizeti na pilipili na kuwasihi wakulima kuchangamkia fursa hiyo.

Alisema pia alishiriki mkutano wa viongozi wa nchi zenye Uchumi Mkubwa Duniani (G20), ambao pamoja na mambo mengine uliazimia kuunga mkono jitihada za upatikanaji wa nishati safi na uwekezaji kwenye kilimo ili kuondosha njaa na umaskini duniani.

UCHUMI KUIMARIKA

Aidha, alisema uchumi wa nchi uliendelea kuimarika na kuwanufaisha wananchi. Kati ya Januari hadi Juni 2024 ulikua kwa asilimia 5.4 ikilinganishwa na asilimia 4.8 katika kipindi kama hicho mwaka 2023.

Alisema deni la taifa liliendelea kuwa himilivu, mfumuko wa bei ukibaki ndani ya lengo la asilimia tatu, hali iliyochangiwa na sera madhubuti za kifedha na ongezeko la uwekezaji ndani na nje ya nchi.

Alisema kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania, kati ya Januari hadi Novemba 2024, serikali ilisajili miradi ya uwekezaji 865 yenye thamani ya Dola za Kimarekani bilioni 7.7 inayotarajia kuzalisha ajira 205,000.

Alisema pia Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Uzalishaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA), ilitoa vibali vya kuwekezwa nchini viwanda vipya vikubwa 15 vyenye thamani ya Dola za Marekani milioni 235, vinavyotarajia kuzalisha ajira karibu 6,000 na kuuza nje bidhaa zenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 94 kwa mwaka.

Alisema Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imefanikiwa kukusanya Sh. trilioni 21.276 kati ya mwezi Januari na Oktoba, 2024 sawa na asilimia 99.3 ya lengo, likiwa ni ongezeko la asilimia 17.5 ikilinganishwa na makusanyo katika kipindi kama hicho mwaka 2023.

Alisema kuimarika kwa uchumi kumeiwezesha nchi kuendelea kufanya mabadiliko chanya katika mifumo ya elimu msingi, sekondari na vyuo vya ufundi, kusogeza huduma bora za afya karibu zaidi na wananchi na kusambaza umeme vijijini

Aidha, serikali imetekeleza dhamira ya kumtua mama ndoo kichwani, kwa kusimamia miradi 1,300 ya maji nchi nzima na kufikisha kutimiza lengo la asilimia 95 mijini na asilimia 85 vijijini.

Alisema serikali pia ilifanikiwa kuhamasisha kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara, kuboresha mifumo ya masoko ya mazao mbalimbali, na kupata bei nzuri ya mazao kwa wakulima.

“Kwa mfano, kwa mwaka 2024 ufuta uliuzwa Sh. 4,850 kwa kilo ikilinganishwa na Sh. 3,600 mwaka 2023, kahawa aina ya arabika iliuzwa Sh. 8,500 kwa kilo ikilinganishwa na Sh. 6,500 mwaka uliopita na kwa kahawa aina ya robusta iliuzwa kwa Sh. 5,000 kwa kilo badala ya Sh. 3,500 mwaka 2023,” alisema.

Alisema pia mbaazi iliuzwa Sh. 2,236 kwa kilo badala ya Sh. 2,000 mwaka 2023, kakao iliuzwa Sh. 35,000 kwa kilo ikilinganishwa na Sh. 29,500 mwaka uliopita na korosho iliuzwa kwa Sh. 4,195 mwaka 2024 ikilinganishwa na Sh. 2,190 mwaka 2023.

Alisema uzalishaji wa korosho unatarajiwa kufikia tani 425,205 kwa msimu wa 2024/2025 unaoendelea ikilinganishwa na tani 310,787 zilizozalishwa msimu uliopita wa 2023/2024.

Alitaja baadhi ya miradi ya kimkakati ambayo imeshaanza kutoa huduma kuwa ni Bwawa la Mwalimu Nyerere ambalo linazalisha umeme Megawatt 3,169 ikilinganishwa na mahitaji ya Megawatt 1,888 huku Reli ya Kisasa (SGR), ikitoa huduma kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma.

Alisema Shirika la Reli lililokuwa linasafirisha wastani wa abiria laki tatu hadi nne kwa mwaka ndani ya miezi mitano ya huduma za SGR, limesafirisha zaidi ya abiria 1,200,000.

Upande wa anga kumekuwa na mafanikio makubwa kutokana na mwaka huu Shirika la Ndege kufikisha ndege 16, kuongeza safari za ndani ya nchi na kimataifa kufikia 25, na kusafirisha zaidi ya abiria 1,1000,000 na tani 10,000 za mizigo.

Alisema serikali pia iliendelea kuboresha mifumo kwenye viwanja vya ndege na ujenzi wa viwanja vya ndege vya Arusha, Kahama, Mpanda na Songwe na mwakani inatarajia kukamilisha viwanja vya ndege vya Iringa, Mtwara, Songea, Kigoma, Msalato, Musoma, Shinyanga na Sumbawanga.

“Hapa nataka nisisitize kuwa, miradi hii ni yetu sote, na imejengwa kwa kutumia rasilimali zetu. Hivyo, tunawajibika kuitunza ili itunufaishe sisi na vizazi vijavyo kesho. Vitendo vya kuhujumu miradi hii ni kulihujumu Taifa,” alisema.

Alihamasisha uwekezaji kwa njia ya ubia baina ya serikali na sekta binafsi (PPP) ili kuongeza ufanisi katika uzalishaji na huduma na mpaka sasa kuna jumla ya miradi 74 ya ubia ambayo ipo katika hatua mbalimbali za maandalizi na utekelezaji.

ATHARI ZA KIMAZINGIRA  

Rais alisema katika kukabiliana na athari za mazingira kutokana na matumizi ya kuni, serikali ilizindua Mkakati wa Kitaifa wa Nishati Safi ya Kupikia na kuwaelekeza wahusika wasimamie ipasavyo utekelezaji wake ili kufikia lengo la asilimia 80 ifikapo mwaka 2034.

CHANGAMOTO ZA 2024

Rais alitaja changamoto serikali ilizokabiliana nazo mwaka 2024 kuwa ni athari za mvua za El-nino na Kimbunga Hidaya, iliyosababisha mafuriko, maporomoko na upotevu wa maisha, uharibifu wa makazi, mashamba na baadhi ya miundombinu ikiwamo barabara na madaraja.

Kutokana na hali hiyo taifa lilisimama pamoja kutoa misaada ya kibinadamu kwa wathirika huku serikali ikijenga nyumba 109 za waathirika wa maporomoko ya Hanang’, mkoani Manyara.” 

Kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), serikali ilitumia Sh. bilioni 136 kutengeneza miundombinu iliyoathiriwa na kutenga Sh. bilioni 868 kutekeleza miradi 70 ya kujenga miundombinu katika maeneo mbalimbali yaliyoathiriwa.

Alitaja changamoto nyingine kuwa ni uhaba wa fedha za kigeni, hususan Dola ya Marekani iliyoathiri biashara na uwekezaji, serikali ilikabiliana nayo kwa kuunda kikosi kazi cha wataalam kilichotafiti hali hiyo na kushauri hatua za kuchukuliwa.

“Nafarijika kwamba, kufuatia utekelezaji wa mkakati huo, upatikanaji wa fedha za kigeni umeimarika. Aidha, katika kuchukua hatua za kuuhami uchumi wetu, serikali imefanya uamuzi wa kuweka akiba ya taifa ya dhahabu katika Benki Kuu ya Tanzania, ili kuongeza uhimilivu wa uchumi wetu.”

Alitaja changamoto nyingine kuwa ni ajali ambazo kwa asilimia 97 zilitokana na makosa ya kibinadamu hasa uzembe wa madereva. Takwimu za Jeshi la Polisi Tanzania zinaonesha kuwa kati ya Januari hadi Desemba mwaka huu, kulitokea jumla ya ajali 1,735, kati ya hizo 1,198 zilisababisha vifo vya watu 1,715 wengine 2,719 wakijeruhiwa.

Aliiagiza Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Jeshi la Polisi Tanzania kuongeza mikakati ya kuzuia ajali zinazosababishwa na makosa ya uzembe.

Alisema pia serikali itajenga viwanja na kumbi zenye viwango vya kimataifa ili kuvutia michezo na mikutano ya kimataifa nchini pamoja na ujenzi wa viwanja unaoendelea Arusha na Dodoma kwa ajili ya kujiandaa na mashindano ya CHAN Februari 2025 na AFCON 2027 ambayo Tanzania ni mwenyeji.

Nchi hiyo imeendelea kusimamia utekelezaji wa falsafa ya 4R, inayohimiza maridhiano, ustahamilivu, mageuzi na kujenga nchi pamoja na kuendeleza uhuru wa habari, wa

kujieleza, kutoa maoni kupitia vyombo mbalimbali na wa kukusanyika na kujumuika.

UCHAGUZI MKUU

Rais Samia alisema kuwa mwaka huu ni muhimu kwa maendeleo ya kisiasa na demokrasia kwa sababu utafanyika Uchaguzi Mkuu kuwachagua rais, wabunge na madiwani na kwa upande wa Zanzibar, atachaguliwa rais, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na madiwani. 

Alisema miongoni mwa maandalizi yaliyofanyika ni kurekebishwa kwa Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, na Sheria ya Vyama vya Siasa.

“Ni imani yetu kwamba sheria hizo zitatuongoza vyema katika kusimamia kwa ufanisi chaguzi zijazo. Nitoe rai kwa wananchi na wadau wote wa uchaguzi kuhakikisha tunaidumisha sifa ya nchi yetu ya kuwa na demokrasia iliyojengeka juu ya msingi wa uhuru na haki,” alisema.