Kanisa lashtushwa na kasi ya mauaji, lasema ni chanzo cha laana katika ardhi

By Mary Mosha , Nipashe
Published at 06:02 AM Dec 08 2024
PAROKO wa Parokia Teule ya Kifuni,Padri Festo Tingo.
Picha:Mtandao
PAROKO wa Parokia Teule ya Kifuni,Padri Festo Tingo.

PAROKO wa Parokia Teule ya Kifuni,Padri Festo Tingo, amesema mauaji yamekuwa tatizo Tanzania, hivyo kuna haja ya jamii kujitafakari kwa sababu husababisha laana katika ardhi.

Alisema hayo jana katika ibada ya maziko ya Isaack Mallya, ambaye ni kaka wa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafi, aliyeuawa kikatili kwa kucharangwa mapanga kichwani na shingoni baada ya kuvamiwa nyumbani na watu wasiojulikana.

“Kila siku ukifungua vyombo vya habari hapa nchini  utakutana na mauaji. Mume  kumuua mke, mke kamuua mume, watoto kuua wazazi, jirani kuuawa. Hii yote ni kutokana na chuki, hasira na kutaka kulipiza kisasi,” alisema.

Desemba 2, mwaka huu, majira ya asubuhi, watu wasiojulikana walivamia nyumbani kwa Mallya wakati akijiandaa  kwenda ibada ya misa takatifu katika Kijiji cha Umbwe Onana, Kata ya Kibosho Magharibi, mkoani Kilimanjaro na kumpiga maeneo mbalimbali ya mwili ikiwamo kichwani. 

Kutokana na hali hiyo, alisema kuna haja ya jamii kujitafakari kwa sababu mauaji hayo huleta laana katika ardhi na hivyo kuleta madhara makubwa kwenye vizazi vyao.

“Kila mmoja aliyefika hapa (kwenye maziko) ajitafakari amekuwa muuaji mara ngapi kwa kulipiza kisasi,  kujenga chuki,  hasira, kutamka maneno ya uongo na matamshi ya kuuwa kwa watu wetu wa karibu.

“Kuhusu tukio hili, polisi tunaamini mtatenda haki na ninyi mtoe ushirikiano ili haki itendeke lakini niwasisitize tutoe ushirikiano. Tuache  kutaka fedha za haraka bila kufanya kazi, "alisema Padri Tingo.

Aliwataka vijana kupenda kufanya kazi na kuridhika na wanachopata na kuhakikisha wanakuwa na nidhamu ili kuleta mabadiliko katika maisha yao.

"Vijana fanyeni kazi. Akili  isiyofanya kazi ni karakana ya shetani. Pendaneni, heshimianeni, msitafutane tu kwa vikao vya send off (sherehe ya kumuaga binti anayeolewa), harusi, msiba na sherehe. Badala yake itaneni  msaidiane, onyaneni, saidianeni na hakikisha mnaleta mabadiliko ya kifikra, 

“Na nyinyi wanandoa, hakikisheni  ndoa zetu zinakuwa mifereji ya kwenda mbinguni. Acheni  kutukanana na kutishiana kila siku nitakuuwa, Hebu waombeeni baraka," alisema.

Akitoa salama za pole kwa familia, mwanaharakati Vick Massawe, alitaka viongozi wa serikali kuchukua hatua  hasa kwa baadhi ya vijana wanaofanya uhalifu na  wanaotumia dawa za kulevya aina ya bangi, pombe  kupitiliza walioko katika Kata ya Kibosho Magharibi. 

"Katika kata hii, bangi inauzwa kama njugu. Ukienda  kuripoti polisi kabla hajafika tayari mtuhumiwa kashafika hali  inayofanya watu kutishwa ndiyo maana ndani ya nyumba yake mmekuta RB nyingi  kwani alikuwa anatoa taarifa kila wakati.

“Katika kata hii, hiki ni kifo cha 12 kwa muda mfupi tu. Polisi  mtusaidie kupata haki na matukio haya yageuke kuwa historia,"alisema. 

Katibu Tawala Mkoa Kilimanjaro, Kiseo Nzowa,  alilitaka Jeshi la Polisi  kuhakikisha watuhumiwa wanakamatwa na kuwaomba wananchi kutoa taarifa ili zisaidie upatikanaji wa haki.

"Wananchi ni lazima tutunze amani, tutoe taarifa tunajua kuwa mnawajua na mnaishi nao,  na tujue kuwa kutoa taarifa ni kumaliza tatizo.

“Haya mambo ya mauaji tusiyaone ya kawaida hata kidogo, tujiepushe na migogoro, chuki, na visasi haviwezi kutusaidia chochote katika maisha yetu, na tutambue tusipotoa ushirikiano kesho litakuja kwako, hawa ni vijana wetu wanaotekeleza matukio hayo," alisema. 

Kamanda wa Polisi Mkoa Kilimanjaro, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Simon Maigwa, alisema tayari wamewakamata watu wanne kuhusiana na tukio hilo na kuitaka jamii kama ina taarifa yoyote ya ziada iwasilishwe kituoni.

"Tangu tulipopata taarifa hizi, tumefanya msako mkali na tumewakamata watu wanne na tunaendelea kwa uchunguzi, tunawaomba yeyote  mwenye taarifa ya ziada asisite kuitoa.

“Ila jamiii  tunaomba ushirikiano wenu. Vijana  hawa ni wetu na hapa nimesikia kuwa huyu ni mtu 12 kuuawa,  sijui ni kabla sijaja au la. Ila   ninaomba  vyombo vyangu tutayafanyia kazi, haki itapatikana, niwahakikishia mkoa uko salama sana,"alisema Kamanda Maigwa.