Jalada la 'Afande' vijana kubaka 'Binti wa Yombo' latua kwa DPP

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 04:40 AM Aug 25 2024
 Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) David Misime
Picha: Mtandao
Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) David Misime

JALADA kuhusu tuhuma za anayedaiwa afande wa jeshi kutuma vijana kubaka na kulawiti binti anayedaiwa mkazi wa Yombo Dovya, mkoani Dar es Salaam, limetua kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP).

Jeshi la Polisi limesema kuwa tayari jalada hilo linalomhusisha Fatuma Kigondo, anayetuhumiwa kutuma vijana hao, liko mikononi mwa DDP kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria. 

Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) David Misime, aliyasema hayo jana wakati akizungumzia kuhusu tukio hilo na matukio mengine ya watu kuuawa baada ya awali kuripotiwa kupotea na kutekwa. 

"Jeshi la Polisi linapenda kutoa taarifa kuhusu Ofisa wa Polisi anayetajwa kwa jina la Fatuma Kigondo kwamba, uchunguzi wa kina ulishafanyika ikiwa ni pamoja na kupata maelezo ya watu mbalimbali na maelezo yake na jalada vimepelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka," alisema. 

Agosti 4 mwaka huu, katika mitandao ya kijamii, kulisambazwa video ikionesha namna vijana watano wakimfanyia ukatili huo binti huyo huku wakimrekodi. 

Katika video hiyo, vijana hao walisikika wakimtuhumu kutembea na mume wa mtu na binti huyo kusikika akiomba msamaha mtu aliyetambulishwa kama afande. 

Tayari kuna kesi mahakamani mkoani Dodoma inaendelea dhidi ya watuhumiwa wa ukatili huo huku kukiwa na shinikizo 'afande' anayedaiwa kuwatuma, naye afikishwe mahakamani. 

Baadhi ya mawakili pia wamefungua kesi jijini Dodoma dhidi ya Fatuma, wakimhusisha na ukatili huo.  

Hata hivyo, kwa sheria za Tanzania, mamlaka ya kuchunguza, kukamata na kushtaki mtu kwa kesi ya jinai yako kwa Jeshi la Polisi na mamlala linazoshirikiana nazo, ikiwamo ofisi ya DPP. 

Tukio hilo la binti kutendwa ukatili huo, liliibuliwa na aliyekuwa Meya wa Ubungo, Boniface Jacob wiki mbili zilizopita ambaye aliandika mkasa mzima kwenye ukurasa wake wa X huku akiwatumia nakala, Rais Samia Suluhu Hassan kama Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi Tanzania, Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Stergomena Tax na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dorothy Gwajima.

 Boniface aliandika: "Binti huyu amebakwa na kulawitiwa akiwa anarekodiwa video tatu tofauti. Askari hao walimrekodi wakiwa wanambaka na kumlawiti, wamesambaza video zake mitandaoni kwa maagizo ya kiongozi wao (afande) ambaye amewatuma kumpatia huyu binti adhabu. 

Kwa mujibu wa Sheria ya Kanuni za Adhabu, Sura ya 16, kosa la kubaka kwa kikundi, adhabu yake ni kifungo cha maisha gerezani, hivyo washtakiwa hao wakithibitika kutenda ukatili huo, watakumbana na adhabu hiyo.