WATENDAJI wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura, wameaswa kutekeleza majukumu waliyopewa, kwa kuzingatia sheria, kanuni, maelekezo na miongozo itakayotolewa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).
Wito huo umetolewa na Mjumbe wa INEC Balozi Omari Mapuri, wakati akifunga mafunzo ya watendaji wa uboreshaji wa daftari mkoani Morogoro, leo, Februari 19, 2025.
“Mnapaswa kutekeleza majukumu mliyopewa kwa kuzingatia sheria, kanuni, maelekezo na miongozo itakayotolewa na Tume,” amesema katika mafunzo hayo ya siku mbili.
Balozi Mapuri ametoa wito kwa watendaji hao kuendelea kutumia muda wao wa ziada kusoma na kupitia maelekezo yote waliyopewa, ili kuongeza uelewa zaidi kuhusu wajibu na majukumu yao wakati wa kutekeleza zoezi lililopo mbele yao.
Akifunga mafunzo kama hayo mkoani Tanga, Mjumbe wa Tume ambaye pia ni Jaji wa Mahakama Kuu, Asina Omari, amewataka watendaji hao kusoma katiba na sheria ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
“Someni kwa makini Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Sheria ya Uchaguzi, Kanuni za uboreshaji, Maelekezo na Miongozo yote inayotolewa na Tume, ili kazi yenu ifanyike kwa unadhifu na haki,” amesema.
Jaji Asina amewakumbusha watendaji hao juu ya wajibu wao wa kuhamasisha wananchi wenye sifa, ili wajitokeze kujiandikisha na kupata haki yao ya kikatiba itakayowawezesha kushiriki katika kuchagua viongozi wao kwenye uchaguzi mkuu utakoafanyika mwaka huu.
Uboreshaji wa Daftari utafanyika mkoani Morogoro na kwenye Mkoa wa Tanga katika Halmashauri za Wilaya ya Bumbuli, Handeni, Pangani na Mkinga kwa siku saba kuanzia Machi Mosi hadi 07, 2025 na vituo vitafunguliwa saa 2:00 asubuhi na kufungwa saa 12:00 jioni.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED