Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) imepanga kufanya mnada wa vitalu 26 vya gesi asilia na mafuta mnamo Machi 5, mwaka huu, katika Ukumbi wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam, kwa lengo la kuvutia wawekezaji ili kuchangia maendeleo ya nchi.
Mkurugenzi Mkuu wa PURA, Mhandisi Charles Sangweni, ametoa taarifa hiyo wakati akifungua Mkutano wa Pili wa Baraza la Wafanyakazi wa PURA, unaofanyika mkoani Morogoro.
Amesema kuwa mnada huu ni wa tano kufanyika nchini, baada ya ile ya awali kufanyika katika miaka ya 2000, 2004, 2008, na 2013, ambapo mnada wa mwaka 2013 uliwezesha upatikanaji wa gesi inayotumika katika maeneo mbalimbali nchini.
Mhandisi Sangweni ameongeza kuwa kati ya vitalu 26 vitakavyonadiwa, 23 vinapatikana katika Bahari ya Hindi, huku vitatu vikiwa katika Ziwa Tanganyika. Ameeleza kuwa kutokana na ugunduzi wa gesi katika maeneo hayo, wanatarajia kugundua akiba zaidi.
Kwa sasa, Tanzania ina jumla ya vitalu 8, ambapo vitatu vinazalisha gesi huku vitano vikiwa katika hatua za utafiti. Amesema kuwa baada ya kupata wawekezaji, vitalu vipya vitajumuishwa na vilivyopo, na hivyo kufikia zaidi ya 30.
Aidha, Mhandisi Sangweni amesema kuwa baada ya mnada huo, PURA ina matumaini kuwa ifikapo mwishoni mwa mwaka huu, wawekezaji watakuwa wamepatikana, jambo ambalo litaleta manufaa kwa wananchi na taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga, ameuagiza uongozi na watumishi wa PURA kuendelea kujituma na kuhakikisha kuwa duru ya tano ya uuzaji wa vitalu vya utafutaji wa mafuta na gesi asilia inaleta matokeo chanya. Amesema Wizara ya Nishati itaendelea kuunga mkono juhudi hizo ili kufanikisha malengo yaliyowekwa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED