Kamati ya PIC yaona tija uwekezaji Kiwanda cha uzalishaji bidhaa za ngozi

By Renatha Msungu , Nipashe
Published at 01:39 PM Feb 19 2025
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Ridhiwani Kikwete.
Picha: Mpigapicha Wetu
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Ridhiwani Kikwete.

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na mitaji ya Umma (PIC) imeipongeza serikali kwa uwekezaji wenye tija na manufaa kwa maendeleo ya nchi inayofanya katika kiwanda cha uzalishaji wa bidhaa za ngozi Kilimanjaro International Leather Industries Co Ltd.

Akizungumza mara baada ya kutembelea kiwanda hicho  mwenyekiti wa kamati hiyo  Agustine Holle amesema kuwa kutokana na uwekezaji wenye tija waliouona utaiwezesha  serikali kuongeza  mapato. 

Aidha amesema  kiwanda hicho kitaunufaisha mkoa wa Kilimanjaro pamoja na mikoa ya jirani kwa kuboresha mfumo wa maisha ikiwemo  kuongeza kipato kwa wakazi wa maeneo hayo na nje ya mkoa huo.

Mwenyekiti amebainisha kuwa wameridhika na uendeshaji wa Kiwanda hicho ambapo kitakapokamilika kwa asilimia 100 kinakwenda kutoa ajira 3,000 ambazo ni ajira za moja kwa moja na ajira nyingine zisizo za moja kwa moja ni 4,000.

Kwa upande wake  Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Ridhiwani Kikwete ameihakikishia kamati hiyo kuwa ataendelea kusimamia maono ya Rais  Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuufanya uwekezaji huo wenye  tija unakuwa endelevu kwa manufaa ya watanzania na nchi.