KAMATI ya Olimpiki Tanzania (TOC), imeviagiza vyama na mashirikisho ya michezo nchini kuunda Kamisheni ya Mchezo wao ikiwamo kufuata maelekezo yao ili kuhakikisha taifa linapiga hatua katika sekta hiyo.
Hayo yalisemwa na Katibu wa TOC, Filbert Bayi, wakati wa ufunguzi wa mkutano mkuu wa uchaguzi wa Kamisheni ya Wanamichezo TOC, uliofanyika jijini Dodoma na kuhudhuriwa na wawakilishi wa vyama husika.
Bayi alisema TOC inaamini katika vyama vya michezo kukiwa na Kamisheni ya Wachezaji itasaidia kwa kiasi kikubwa kuibua vipaji vya chipukizi, lakini pia uwapo wa nidhamu kwa wachezaji wa mchezo husika.
"Kamisheni ya wanamichezo ina umuhimu mkubwa kwenye vyama, kwa sababu ina uwezo wa kutoa hoja ya kuboresha michezo kwa faida yao, lakini pia kusimamia nidhamu ya mchezo husika," alisema Bayi.
Alisema wao kama TOC, wako tayari kufanya kazi na Kamisheni ya Wanamichezo hususan katika masuala muhimu ya kupeleka mapendekezo yao kimataifa ili kuhakikisha wanashiriki katika michezo ya kimataifa, ikiwamo kutambulika kupitia vyama husika.
Kutokana na hilo, Bayi alisema, Kamisheni ya Wanamichezo ina uwezo wa kupanua wigo wa kusaidia pia, wachezaji waliostaafu kucheza, kwa kuwatumia kuendeleza vipaji vya wachezaji wanaochipukia ili kuhakikisha wanaendeleza vipaji vyao kutokana na uzoefu waliokuwa nao.
Mbali na hayo, amewataka kuweka jitihada za kutoa ushauri wa kufanya mazoezi kwa wachezaji chipukizi hapa nchini, ili kuhakikisha wanapiga hatua katika michezo wanayofanya ndani na nje ya nchi.
"Kamisheni ya wachezaji mna nafasi kubwa kuhakikisha michezo inasonga mbele kwa sababu mna uwezo wa kushauri viongozi wa vyama na mashirikisho kuhusu maendeleo ya michezo," alisema Bayi.
Naye Rais wa TOC, Gulam Rashid, alisema Kamisheni ya Michezo inapaswa kuwa mstari wa mbele kuondoa migogoro iliyopo ndani ya vyama vya michezo au mashirikisho kwa sababu inachangia kurudisha nyuma maendeleo ya michezo.
Kutokana na hilo, amesisitiza vyama kuunda Kamisheni za Wachezaji ambazo zitakuwa zikiwasaidia wanamichezo kuwasilisha mapendekezo yao kwa ajili ya kuboresha michezo hapa nchini.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED