Simba yapania kukaa kileleni leo

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 09:07 AM Nov 06 2024
Simba yapania kukaa kileleni leo
Picha: Mtandao
Simba yapania kukaa kileleni leo

USHINDI wowote itakaoupata timu ya Simba leo dhidi ya KMC, utaipeleka kileleni kwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, huku Kocha Mkuu Fadlu Davids, akionesha furaha kwa kurejea kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam.

Simba yenye pointi 22, ikiwa nafasi ya tatu ya msimamo, itafikisha pointi 25 kama ikipata ushindi leo na kuishusha Yanga inayoongoza kwa pointi 24, ambayo nayo itasubiri mchezo wake wa kesho dhidi ya Tabora United.

Kocha huyo jana alisema kuwa amefurahi mno kurejea tena hapo kwani ni uwanja wao wa nyumbani, lakini unawaruhusu kucheza aina yoyote ya soka wanalotaka.

Simba inarejea kwenye uwanja huo baada ya kupata tabu Ijumaa iliyopita ikicheza ugenini, Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma na kushinda kwa mbinde bao 1-0 dhidi ya Mashujaa FC, ikilazimika kusubiri hadi dakika ya mwisho ya majeruhi kwa bao la Mganda Steven Mukwala.

Pamoja na mambo mengine kocha huyo alilalamikia pia uwanja kuwa haukuwa rafiki kwa wachezaji wake.

"Matayarisho yamekwenda vizuri, najua mechi itakuwa ya ngumu sana, lakini nimefurahi kurejea kwenye dimba la KMC, uwanja ambao tumeuzoea, tunautumia kama wa nyumbani ambao unaruhusu kucheza soka la aina yoyote tunalotaka," alisema kocha huyo.

Simba inatumia Uwanja wa KMC Complex kama wake wa nyumbani, pia kesho kikanuni itakuwa mwenyeji, lakini uwanja huo ni mali ya Manispaa ya Kinondoni inayoimiliki timu ya KMC.

"Kila mechi iko tofauti na mahitaji yake ni tofauti pia, najua watakuja kwa nguvu kwa ajili ya kutukabili, nimeisoma KMC jinsi gani inavyocheza, wanacheza soka la kushambulia moja kwa moja, hivyo itabidi safu yangu ya ulinzi kuwa makini, hebu tuangalie watakavyoanza ili tujue tukabiliane nao vipi," alisema.

Kiungo mshambuliaji wa Simba, Awesu Awesu anayerejea nyumbani KMC, kucheza na timu yake ya zamani, alisema hawawezi kucheza kama walivyocheza dhidi ya Mashujaa FC, badala yake watabadilika kwenye mfumo.

"Hii ni mechi ya nyumbani, hatuwezi kucheza kama zile za ugenini, kocha ametuelekeza jinsi gani ya kucheza mechi za ugenini hasa kwenye viwanja vya mikoani na tukiwa nyumbani kwenye kiwanja bora tucheze vipi," alisema mchezaji huyo ambaye Simba ilimsajili mwanzoni mwa msimu kutokea timu hiyo.

Naye Kocha Mkuu wa KMC, Abdihamid Moalin, amesema wanatakiwa kucheza kwa umakini na maelewano kwani wanacheza na timu kubwa inayoweza kutumia makosa ya wapinzani kuwaadhibu.

"Mechi itakuwa ngumu, Simba ni timu kubwa, tunatakiwa tucheze kwa umakini na kwa maelewano ya hali ya juu, tunajua tuna mapungufu sehemu ambayo siwezi kuyataja.

Mimi napenda kucheza mpira, napenda wachezaji wangu wainjoi na hiyo ndiyo falsafa ya KMC, nafikiri yeyote atakayefanya makosa mengi ndiye atakayeadhibiwa," alisema kocha huyo.

KMC ipo nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 14 na katika mchezo huo inakwenda kucheza mechi ya 11, huku Simba ikifikisha mechi ya 10.