Simba SC yatua Mali kusajili mshambuliaji

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 11:37 AM Jun 10 2024
 Ibrahim Gadiaga.
Picha: africafoot.com
Ibrahim Gadiaga.

KLABu ya Simba tayari imeanza mikakati ya kukiimarisha kikosi chao kwa kuamua kwenda nchini mali kusajili mshambuliaji atakayewasaidia kuwarudisha kwenye ubora wao.

Simba inatajwa kutaka kumsajili mshambuliaji wa klabu ya FC Nouadhibou ya Mauritania raia wa Mali, Ibrahim Gadiaga.

Habari kutoka ndani ya klabu hiyo zinasema mshambuliaji huyo  amepachika mabao 12 kwenye Ligi Kuu ya Mali akiwa na klabu ya Bakaridjan kabla ya kuhamia nchini Mauritania na kujiunga na klabu hiyo.

"Bado waliopewa dhamana ya kusajili wanahaha huku na kule kusaka mshambuliaji mwenye uwezo mkubwa na siyo kama wale waliokuwapo msimu uliopita, hivi sasa wamekwenda mpaka Mauritania kuulizia uwezekano na kumpata kijana huyu raia wa Mali, ana miaka 19 tu, lakini analijua goli, kama wakifanikiwa na kumpa mkataba mrefu anaweza kuisaidia Simba kwa muda mrefu," kilisema chanzo ndani ya klabu hiyo.

Aidha, taarifa zinasema kuwa tayari kikosi kazi kilichopewa mamlaka ya usajili na Mwekezaji, Mohamed Dewji, kinadaiwa kimeshakubaliana na winga anayeichezea klabu ya AS Vita ya  Jamhuri ya Kidemkorasi ya Kongo, Elie Mpanzu na Derrick Fordjour kutoka Medeama ya Ghana.

Pia Simba inatajwa kumuwinda mshambuliaji Ricky Banda, raia wa Zambia anayeichezea Red Arrows ya nchini humo.

"Rais wa Heshima anataka kurudisha ufalme wa timu, ndiyo maana ameteua kikosi kazi, baada ya kuona kuna watu wanamkwamisha, anatoa pesa, lakini wanaletwa wachezaji wenye viwango vya chini," kilisema chanzo hicho.

Inadaiwa safari hii Dewji mwenyewe yupo mstari wa mbele katika kusajili wachezaji wa viwango vya hali ya juu, akiwaongeza watu wengine kumsaidia kazi hiyo ambao ni Sued Mkwabi, Mulamu, Ng'ambi, Crescentius Magori na Kassim Dewji.

Meneja Habari wa Mawasiliano wa Klabu hiyo, Ahmed Ally alisema mipango yote inatekelezwa kwa ustadi na ufanisi wa hali ya juu.

"Usahihi ni kwamba mipango na mikakati thabiti inaendelea na itakapokua tayari wote watajulishwa.

Jambo la kufurahisha ni kwamba mipango yote inatekelezwa kwa ustadi na ufanisi wa hali ya juu mno, malengo tuliyojiwekea ya kuboresha timu yetu yamefikiwa kwa asilimia kubwa kwa maana ya kwamba mipango yetu kwenye soko la usajili iko vizuri sana.

Niwaombe wanasimba tutulie, la mgambo likilia tutafahamu kila kitu kuhusu timu yetu pendwa," alisema Ahmed.