NAHODHA wa Simba, Mohamed Hussein 'Zimbwe Jr', amefichua malengo ya timu na wachezaji wa timu hiyo waliojiwekea msimu huu ni kufika hatua ya Fainali ya mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika au kulitwaa kombe la michuano hiyo.
Vinara hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara ndio wawakilishi pekee wa Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati waliobakia katika mashindano ya kimataifa yanayosimamiwa na kuandaliwa na CAF.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Zimbwe Jr, beki wa kushoto wa timu hiyo, alisema malengo hayo hayakuwa kutinga robo fainali, bali ni kufika mbali ikiwamo ndoto za kubeba ubingwa.
Nyota huyo alisema kutinga hatua ya robo fainali kwao ni njia ya kupita kuelekea kwenye mafanikio wanayoyahitaji msimu huu.
Alisema yeye binafsi ameweka rekodi ya kufika robo fainali mara sita katika michuano ya kimataifa, hivyo hawezi tena kushtuka akifika hapo, badala yake anataka kusonga mbele zaidi msimu huu.
"Ni jambo kubwa sana kwangu kutimiza robo fainali sita za kimataifa zinazotambuliwa na CAF, kwa sababu wapo ambao wanatamani kuwa hapa, lakini hawafikii malengo.
Niseme tu safari hii siyo tena robo fainali, ni fainali, kuna matarajio yangu binafsi ambayo nataka nivuke hatua ambayo siku zote naishia, malengo ya klabu tuliopewa na viongozi wetu pamoja na yetu sisi wachezaji wote ni kuhakikisha tunafika fainali na ikiwezekana kutwaa taji lenyewe," alisema Zimbwe Jr.
Aliongeza kwa sasa wanafanya mazoezi ya kujiandaa na mechi ya Kombe la FA na Ligi Kuu Tanzania Bara, lakini akiwa na uhakika muda utakapofika wataanza kujiandaa kikamilifu na michezo miwili hatua ya robo fainali.
"Nadhani tukikaribia kucheza robo fainali, Kocha Fadlu (Davids) ataanza kutupa mazoezi yanayoendana na uzito wa michuano hiyo, pamoja na aina ya timu tunayokwenda kucheza nayo kama ambavyo amekuwa akifanya mara zote.
Mchezaji huyo alisema ndani ya kikosi hicho, mbali na kazi yake ya unahodha, moja ya kazi anayoifanya ni kuwafundisha wachezaji wapya utamaduni wa klabu yao na 'kiu' ya kufikia malengo.
"Wachezaji wote wapya wakifika kitu cha kwanza ni lazima ajue utamaduni wa timu, pili malengo ya klabu yakoje na hayo huwa tunapewa na viongozi kabla ya msimu kuanza, kila mchezaji anatakiwa alitambue hilo kila anapokuwa ndani na nje ya uwanja," alisema.
Mchezaji huyo aliyejiunga na Simba mwaka 2014 akitokea Kagera Sugar, amecheza robo fainali sita ndani ya misimu saba, Ligi ya Mabingwa mara nne kuanzia msimu wa 2018/19, 2020/21, 2022/23 na 2023/24, huku kati ya msimu wa 2021/22 na msimu huu, akicheza michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Simba, ambayo ilimaliza kinara wa Kundi A, inatarajia kucheza mechi ya robo fainali dhidi ya Stellenbosch ya Afrika Kusini , Asec Mimosas (Ivory Coast) au Al Masry ya Misri, ambazo zilimaliza kwenye nafasi ya pili kwenye makundi mengine.
Mechi za kwanza za hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika zitachezwa kati ya Machi 28 hadi 30, ambapo Simba ikitarajia kuanzia ugenini huku marudiano yakipangwa kufanyika kati ya Aprili 4 hadi 6, mwaka huu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED