MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya Wanawake nchini (TWPL), Simba Queens, wanatarajia kuikabili Mlandizi Queens, katika mechi ya ligi hiyo itakayochezwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam leo.
Mechi hiyo ambayo awali ilipangwa kuchezwa kwenye Kituo cha TFF Kigamboni saa 10:00 alasiri jana, sasa itachezwa leo kuanzia saa 8:00 mchana.
Akizungumza na gazeti hili jana, Kocha Mkuu wa Simba Queens, Yussif Basigi, alisema kila mechi kwao ni kama fainali na wamejiandaa kupambana kuhakikisha wanapata pointi tatu.
Basigi alisema ligi hiyo inaushindani na ili timu yako ifikie malengo, inahitaji kushinda kila mchezo kwa ajili ya kujiimarisha katika msimamo.
"Tuko tayari kwa mechi ya kesho (leo), ninajua utakuwa mchezo wenye ushindani, ni wazi kila timu ilitumia muda wa mapumziko kujiimarisha, wakati wote mechi za mzunguko wa pili huwa ni ngumu kwa sababu ni wakati wa kurekebisha makosa ya nyuma, na ukitaka ubingwa ni lazima ushinde mechi zako," alisema Basigi.
Aliongeza kuwa anafurahia kuona ushindani unaongezeka katika kikosi chake kwa sababu kila mmoja anataka kupata namba kwenye kikosi cha kwanza.
"Lakini kutafuta nafasi ya kuitwa katika timu za taifa ni jambo linalosaidia kukuza viwango, wachezaji wanafahamu umuhimu wa kuchezea timu za taifa, kwetu ni jambo zuri na linasaidia kutupa matokeo chanya katika michezo ya ligi ya hapa Tanzania, tunaamini tutazidisha kujituma ili kutetea ubingwa," Basigi alisema.
Simba Queens ndio vinara wa ligi hiyo wakiwa na pointi 25, wakifuatiwa na JKT Queens yenye pointi 22, lakini imecheza mchezo mmoja pungufu wakati Mlandizi Queens inaburuza mkia ikiwa na pointi moja.
Wakati huo huo, Yanga Princess, imeendelea kuimarisha kikosi chake kwa kutangaza kumsajili Mchezaji Bora wa Ligi Kuu ya Wanawake Kenya msimu uliopita, Lidya Akoth.
"Tunapenda kutangaza rasmi Lidya Akoth ni Mwananchi," taarifa rasmi katika ukurasa wa Yanga Princess, ilisema.
Katika hatua nyingine, kiungo wa zamani wa Timu ya Soka ya Taifa ya Wanawake (Twiga Stars) na Simba Queens, Kadosho Shabani, amesajiliwa na Fountain Gate Princess ya jijini Dodoma.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED