Simba, Pamba Jiji kibaruani

By Faustine Feliciane , Nipashe
Published at 10:48 AM Nov 22 2024
Simba, Pamba Jiji kibaruani
Picha:Mtandao
Simba, Pamba Jiji kibaruani

SIMBA inatarajia kuutumia mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Pamba Jiji FC utakaochezwa leo kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini, Mwanza kama sehemu ya maandalizi ya mechi ya mashindano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika, imeelezwa.

Mechi hiyo ya kwanza ya hatua ya makundi ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya wageni FC Bravos do Maquis kutoka Angola itachezwa Novemba 27, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Akizungumza na gazeti hili jana, Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, amesema mchezo dhidi ya Pamba Jiji kwao ni kipimo na maandalizi mazuri zikiwa zimebaki siku chake kukutana na Bravos do Maquis.

Fadlu alisema baada ya mapumziko mafupi ya Kalenda ya Kimataifa kumalizika, walihitaji angalau mchezo mmoja wa ushindani na wanafurahia kukutana na Pamba Jiji kwa sababu itawajenga wachezaji wake.

Kocha huyo alisema amejiandaa kukutana na upinzani katika mechi hiyo kwa sababu anafahamu ni 'hatari' kukutana na timu ambayo haina matokeo mazuri katika michezo yake iliyotangulia.

"Mchezo huu wa kesho (leo), ni muhimu sana kwetu, kwanza tunataka kuendelea kujiimarisha kileleni katika msimamo wa Ligi Kuu, lakini pia ni sehemu ya maandalizi yetu kuelekea mchezo wa kimataifa," alisema Fadlu.

Kocha huyo alisema wamejiandaa vizuri na mchezo huo na wanafahamu Pamba wataingia uwanjani kuonyesha upinzani wakijaribu kutafuta ushindi wa kwanza kwenye uwanja wao wa nyumbani.

"Hautakuwa mchezo mwepesi hata kidogo, Pamba wana kocha mzuri na wachezaji wazuri pia, lakini sisi lengo letu ni kuondoka na pointi tatu, ushindi utatuongezea morali zaidi kuelekea katika mchezo wetu wa kimataifa wa CAF," alisema Fadlu.

Aliongeza wachezaji wake wapo katika  hali nzuri na hata waliotoka kwenye majukumu ya kimataifa pia wako tayari kwa ajili ya mchezo huo.

Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amewataka waamuzi wa mchezo huo kuwa makini na kuwaepusha wachezaji wao kuumia.

"Tunaomba Pamba wacheze mpira, wasiingie uwanjani kwa lengo la kuwaumiza wachezaji wetu, tuna mchezo mkubwa wa kimataifa, waamuzi nao wawalinde wachezaji wetu, tuache soka lichezwe uwanjani si kukamiana na kuumizana," alisema Ahmed.

Naye Kocha Mkuu wa Pamba Jiji, Fred Minziro, ameliambia gazeti hili anaiheshimu Simba kutokana na kuundwa na wachezaji wenye uzoefu lakini watahakikisha wanapambana kupata pointi tatu.

"Simba ni timu kubwa na ina wachezaji wazuri kama Pamba Jiji, tumejiandaa kukabiliana nao, tunataka kufanya vizuri kwenye uwanja wetu wa nyumbani," alisema Minziro.

Alisema licha ya kuwa kwenye uwanja wao wa nyumbani, wataingia katika mchezo huo kwa tahadhari na wataongeza umakini ndani ya dakika zote.

Ligi hiyo itaendelea tena kesho kwa KenGold kuikaribisha Coastal Union wakati Mashujaa itawaalika Namungo na Azam itawavaa Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Azam Complex.

Simba yenye pointi 25 ndio vinara wa ligi hiyo yenye timu 16 wakifuatiwa na mabingwa watetezi, Yanga yenye pointi 24 wakati Singida Black Stars iko katika nafasi ya tatu na pointi zake 23 kibindoni huku Azam FC yenye pointi 21 wakikamilisha nne bora.

Kagera Sugar yenye pointi nane sawa na Pamba Jiji na KenGold ilijikusanyia pointi tano tu mpaka sasa ndio zinaburuza mkia kwenye ligi hiyo inayoshirikisha timu 16 kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara.