CCM wapeana tahadhari Uchaguzi wa Mitaa

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:53 AM Nov 22 2024
Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi.
Picha:Mtandao
Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi.

KAMPENI za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa zimeshika kasi kwa viongozi wa kitaifa na makada wa vyama vya siasa kusaka kura za wenyeviti wa vijiji, mitaa na wajumbe.

Kanda ya Ziwa, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimewatuma Katibu Mkuu wake, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi kufungua kampeni Mwanza, Ally Hapi (Kagera), Hussein Bashe (Shinyanga), Issa Gavu (Geita) na Dk. Doto Biteko (Mara).

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) nacho kimewanyanyua vigogo wao, wakianzia mkoa wa kimkakati Mara ambako Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Tanzania Bara, Tundu Lissu anafanya operesheni Tarime Mjini, Nyamongo na baadaye Mwanza. 

Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu jana alikuwa mjini Bunda, Dutwa, Lamadi na alitarajiwa kuingia Kahama mkoani Shinyanga na Mwenyekiti Kanda ya Victoria, Ezekia Wenje pamoja na Mwenyekiti wa Baraza la Vijana CHADEMA (BAVICHA), John Pambalu wanaendelea kushambulia maeneo yaliyosalia katika kanda hiyo.

Mkoani Mwanza, Balozi Dk. Nchimbi alihimiza wanachama na viongozi kutambua mtaji wa imani walionao kwa watanzania na wazingatie mambo manne kuibuka washindi katika uchaguzi huo. 

Aliwataka kukomaa na kampeni za nyumba kwa nyumba, mtu kwa mtu. Kuomba kura kwa wanachama na viongozi wa upinzani ili wawaunge mkono. 

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), Hussein Bashe, akizindua kampeni hizo wilayani Kishapu, mkoani Shinyanga, alisema chama hicho tayari kimeshinda kwa asilimia 77 na kitahakikisha kinaendelea kuwalinda na kuwatetea wakulima ili kuhakikisha kilimo kinawanufaisha.

Mkoani Kagera, Katibu wa Jumuiya ya Wazazi CCM Taifa, Ally Hapi aliwataka wananchi kuchagua viongozi ambao watawasaidia katika kuwaletea maendeleo na kutatua matatizo yaliyoko katika maeneo yao.  

Mwenyekiti wa CCM Mkoa Kagera, Nazri Karamagi alisema mkoa huo una kata 192, vijiji 662, mitaa 66 na vitongoji 3,662, hivyo kutaka umoja katika kuhakikisha chama hicho kinachukua nafasi zote.  

Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC) Oganaizesheni na Mjumbe wa Kamati Kuu, Issa Gavu, akizindua kampeni hizo mkoani Geita, alisema wananchi wanatakiwa kukichagua chama hicho ili kusukuma maendeleo yao na taifa kwa ujumla. 

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, John Mongella, aliwataka wafuasi wa chama hicho kutofurahia migogoro inayofukuta ndani ya vyama vya upinzani au kusambaratika kwa vyama hivyo, akisisitiza kuwa vyama hivyo ni muhimu kwa maendeleo ya taifa.

Alitoa kauli hiyo juzi jijini Mbeya alipokuwa akizindua kampeni hizo kimkoa, akisema vyama vya upinzani ni muhimu katika kukuza demokrasia ya nchi. 

Alisema agizo hilo ni sehemu ya utekelezaji wa 4R zilizoasisiwa na Rais Samia Suluhu Hassan ambazo lengo lake ni kulifanya taifa kuwa na utulivu ili maendeleo yapatikane kwa haraka. 

CHADEMA 

Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Victoria, Ezekia Wenje akizinduzi kampeni jijini Mwanza, aliahidi kuwa chama hicho hakitokata tamaa licha ya wagombea wake kuenguliwa katika kinyang'anyiro.

"Lengo ni kutufanya tukate tamaa lakini kwa kipindi hiki hatukati tamaa, bali tunaendelea mpaka kieleweke na kwa wale ambao wanashawishiwa waendelee kuweka msimamo kwani hii ni kazi ya kitume," amesema Wenje.

Mwenyekiti wa BAVICHA, Taifa John Pambalu alizinduzi kampeni hizo katika Kata ya Mahina, Butimba, Igogo na Mabatini jijini, aliwataka wananchi kushiriki kikamilifu katika upigaji kura utakaofanyika Novemba 27, 2024.  

AAFP, NLD

Chama cha Wakulima (AAFP) kimesema kitanadi sera zake kwa kuwafikia wananchi nyumba kwa nyumba na kuwahamasisha kujitokeza kwa wingi kwenda kuwapigia kura viongozi wanaowataka.  

Naibu Katibu Mkuu Taifa Maik Mhomela, alisema jana kuwa wanaamini kampeni hizo zitawafikia hata wale wasiotaka kwenda kusikiliza kwenye mikutano ya hadhara.

Chama cha The National League for Democracy (NLD), kilizindua kampeni zake jana kikitamba kitasaidia kutanua wigo wa ajira na maendeleo nchini, na kulaani vikali serikali kuwatumikisha kazi ngumu, ikiwamo kuchimba mitaro, visima na mabwawa wananchi waliomo katika programu za kupunguza umasikini nchini.

Uzinduzi wa kampeni zake zimefanyika katika Kijijij cha Kwedikwazu wilayani Handeni, mkoani Tanga ambako Katibu Mkuu wa NLD, Doyo Hassan Doyo alisema, "Kijiji hiki tumesimamisha wagombea. Kijiji hiki kina madini lakini kwenye akaunti ya kijiji hakuna hata mia mbovu, mana yake uongozi uliokuwapo madarakani umeshindwa kusimamia maslahi ya wakazi wa kijiji hiki."

ACT WAZALENDO

Kiongozi mstaafu wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, aliwataka wananchi wa kijiji cha Ilalanguru, Jimbo la Kigoma Kusini, mkoani Kigoma kuchagua viongozi wanaowajibika. 

Akihutubia wananchi katika mkutano wa hadhara jana, Zitto alisema kwenye maeneo ambayo wagombea wa vyama vya upinzani wameenguliwa na kubakia wa CCM, wawapigie kura ya 'HAPANA'.

"Miaka mitano iliyopita, uchaguzi kama huu tunaoifanya ulivurugwa, watu wakapitishwa bila kupingwa, wakatangazwa kuongoza vijiji na mitaa yetu bila ridhaa yenu. 

"Mwaka huu figisu zipo, watu wameenguliwa lakini hakuna aliyetangazwa kupita bila kupingwa kwasababu chama chenu cha ACT Wazalendo kilichukua hatua muhimu sana," alisema. 

Katibu wa NEC Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla, alisema jijini Dar es Salaam kuwa watakaoshinda kwa haki katika uchaguzi huo watatangazwa.

"Uchaguzi huu tunakwenda kupata viongozi tunaokwenda kuishi nao kila siku. Uchaguzi huu ni muhimu ili Rais Samia Suluhu Hassan akileta fedha za zahanati, viongozi hawa ndio wanaohusika. 

"Lazima mwangalie ni aina gani ya wagombea ambao tukiwachagua watakuwa suluhisho la matatizo yetu na tutashirikiana nao. Tumewaletea wagombea wazuri watatuzi wa kero zetu," alisisitiza.

Mwenyekiti CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Abbas Mtemvu, alisema chama kimeleta watu wazuri na wana uhakika watafanya kazi vizuri chini ya Rais Samia, wabunge na madiwani.  

*Imeandikwa na Vitus Audax, Rose Jacob (MWANZA), Marco Maduhu (SHINYANGA), Restuta Damian (KAGERA), Alphonce Kabilondo (GEITA), Paul Mabeja, Peter Mkwavila, Renatha Msungu (DODOMA),Elisante John (SINGIDA), Boniface Gideon (HANDENI), Nebart Msokwa (Mbeya), Restuta James na Romana Mallya (DAR) na Mussa Mwangoka (KATAVI).