Benki Kuu: Wakopeshaji hawa 69 hatuwatambui

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 12:14 PM Nov 22 2024
Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba.
Picha: Mtandao
Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba.

MWEZI mmoja baada ya Nipashe kutoa ripoti kuhusu utoaji mikopo holela unaofanywa mtandaoni, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imetangaza orodha ya watoa huduma 69 wasiokuwa na kibali ambao hawaruhusiwi kutoa huduma za mikopo mtandaoni.

Oktoba 21 mwaka huu, Nipashe ilichapisha ripoti ya uchunguzi, ikionesha madhila wanayokutana nayo wakopaji mtandaoni, huku BoT ikieleza kuwa haiwatambui kisha ikatoa mwongozo na kuwataka wajisajili ndani ya siku 14.

Licha ya BoT kutoa mwongozo huo na kuagiza wajisajili, ni watoa huduma wanne tu walijitokeza kusajiliwa ambao Benki Kuu haijawaweka wazi.

Taarifa kwa umma iliyotolewa jana na Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba, ilibainisha kuwa: "Benki Kuu ya Tanzania inapenda kufahamisha umma kuwa imebaini kuwapo kwa majukwaa na programu tumizi (applications) zinazojihusisha na utoaji mikopo kidijitali bila ya kuwa na leseni na idhini kutoka Benki Kuu ya Tanzania."

Kupitia taarifa yake hiyo, Gavana Tutuba alisema majukwaa na programu hizo zimeshindwa kukidhi matakwa ya Mwongozo kwa Watoa Huduma Ndogo za Fedha wa Daraja la Pili wanaotoa huduma za mikopo kwa njia ya kidijitali wa mwaka 2024 uliotolewa na BoT.

"Mwongozo huo unalenga kuimarisha usimamizi wa Watoa Huduma Ndogo za Fedha Daraja la Pili nchini na kuhakikisha uzingatiwaji Kanuni za Kumlinda Mlaji wa Huduma za Fedha, ikijumuisha uwazi, uwekaji tozo na riba, njia za ukusanyaji madeni, na utunzaji taarifa binafsi za wateja na kulinda faragha zao," alisema. 

Gavana Tutuba alisema, "Kupitia taarifa hii, Benki Kuu ya Tanzania inapenda kuarifu umma kwamba majukwaa na programu tumizi zifuatazo hazina kibali na haziruhusiwi kuendelea na shughuli za utoaji mikopo kidijitali.

"Applications hizo ni BoBa Cash; Hewa Mkopo; Money Tap; Soko loan; Bolla Kash Financial Credit; Hi Cash; Mpaso Chap Loan-Mkopo Kisasa; Sunloan; BongoPesa-Personal Online Loan; HiPesa; Mun loan; Sunny Loan na Cash Mkopo.

"Wengine ni Jokate Foundation Imarisha Maisha; My credit; Swift Fund; Cash pesa; KOPAHAPA; Nikopeshe App; TALA; Cash poa; Kwanza loan;  Nufaika Loans; TikCash; CashMama; L-Pesa Microfinance;  Okoa Maisha – Mkopofast na Twiga Loan.

"Wengine ni CashX; Land cash; Pesa M; TZcash;  Credit Land; Loanplus; Pesa Rahisi; Umoja; Eaglecash TZ;  M-Safi;  PesaPlus 64. Usalama Na Uwakika Mkopo Dk15; Fast Mkopo 29. 

"Wengine ni Mkopo Express; PesaX ; Ustawi loan; Flower loan; Mkopo Extra; Pocket loan;  Viva Mikopo Limited; FUN LOAN; Mkopo haraka;  Pop Pesa; VunaPesa; Fundflex; MkopoFasta;  Premier loan; Yes Pesa; Get cash.

"Wengine ni MkopoHaraka; Safe pesa; ZimaCash; Getloan; Mkopohuru; SasaMkopo; Getpesa Tanzania; Mkoponafuu; Silk loan; Hakika loan;  Mkopowako na Silkda Credit."

Gavana Tutuba alisema BoT inatahadharisha umma kutojihusisha na majukwaa na progamu tumizi hizo na inashirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuzifungia programu hizo ili kuepusha umma kutumia huduma za fedha zisizokuwa na vibali vya mamlaka husika. 

"Benki Kuu Tanzania imechapisha na itaendelea kuhuisha orodha ya watoa huduma walioidhinishwa kutoa huduma za mikopo katika tovuti yake," alisema Gavana.

Katika tovuti ya BoT, kumewekwa pia orodha ya watoa huduma ndogo za fedha waliosajiliwa 1,957 na 12 ambao wamenyang’anywa leseni kwa kushindwa kukidhi matakwa ya leseni zao.

Walionyang’anywa leseni kwa maeneo wanayotoka na idadi kwenye mabano ni Shinyanga (1), Kinonndoni (4), Ilala (3), Ubungo (2), Arusha (1) na Karatu (1).

Katika uchunguzi wake, Nipashe ilibaini watoa mikopo mtandaoni, wengi wao ni waliosajiliwa na BoT kama watoa huduma ndogo za fedha (microfinace) ambao wanamiliki programu tumizi.

Nipashe ilibaini wanatoa mikopo yenye riba kubwa inayofika hadi asilimia 80, masharti ya mikopo yanafichwa, udhalilishaji wakopaji kwa kuundiwa makundi katika mitandao ya kijamii kisha picha zao kusambazwa na matumizi ya namba za simu zenye utambulisho (code) usiotambulika.

Nipashe pia ilibaini vijana wenye umri mdogo wamekuwa wanatumika kutukana na kudhalilisha wakopaji kwa njia ya simu, kutuma na kusambaza picha chafu zilizotengenezwa kwa lengo la kushinikiza mkopaji kulipa kiasi kisichostahili, wakopaji kupewa mkopo pungufu kinyume cha makubaliano ya awali na kuwapo raia wa China wanaotumia teknolojia kutoa mikopo hiyo.