WAMILIKI wa kati na Wadogo wa Malori Tanzania (TAMTOA) wamejitokeza KITUO cha Ubia wa Sekta ya Umma na Binafsi (PPPC), kuonyesha nia yao ya kuwekeza katika Usafiri wa Mwendokasi Dar es Salaam (UDART).
Viongozi na baadhi ya wanachama wa TAMTOA wamezungumza leo na Mkurugenzi Mtendaji wa PPPC, David Kafulila wakimweleza nia yao ya kuwekeza kwenye mradi huo mkubwa wa usafirishaji Dar es Salaam ambao unaendelea kutekelezwa kwa awamu sita tofauti.
Mwenyekiti wa TAMTOA, Chuki Shaban amesema wao ni watu wenye elimu ya kazi hivyo mchakato mrefu hawawezi, hivyo wanatamani kupewa utaratibu mzuri wa kufanikisha lengo lao.
Mjumbe wa Kamati kuu ya TAMTOA, Josephat Pallangyo amesema anafikiri ni vyema utaratibu wa kuwekeza kwa hisa kama ilivyo kwa Benki ya CRDB au NMB ungewekwa.
" Mabasi ya mwendokasi ni uwekezaji mkubwa lakini kwa utaratibu huo uliofanywa kwa benki, sisi kama wasafirishaji hatuna haja ya kuwa na wawekezaji wa nje kwa kuwa uwezo tunao, management iwe nzuri tu, "amesema.
Mkurugenzi Kafulila aliwashauri kuandaa andiko lao jinsi gani wamejipanga kuwekeza pia uwezo wao ni kununua mabasi mangapi, na huduma nyingine ambazo zipo na wameziona kuwa ni fursa.
'Hadi sasa mradi huo katika Awamu ya kwanza na pili zimekamiliki, hivyo wanaweza kuomba kuanzisha Awamu ya tatu na watapewa nafasi wakionyesha jinsi wanavyoweza kutoa huduma zao kulingana na utaratibu uliowekwa,"amesema.
Pia amewashauri kuanzisha kampuni ya umiliki wa pamoja, kisha wawekeze ambapo mtu atavuna faida iliyopatikana kulingana na kiwango cha hisa anazomiliki, lengo la serikali ni kuhakikisha huduma nzuri zinapatikana kulingana na mradi husika.
Septemba 02,2024 Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa (TAMISEMI) Mohamed Mchengerwa, amesema hakuna haja ya kusubiri wawekezaji wa nje katika kupata mabasi ya mwendokasi kwa huduma za mradi huo.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED