THRDC yawapiga msasa mawakili kuelekea uchaguzi

By Pilly Kigome , Nipashe
Published at 05:37 PM Nov 22 2024
 Mratibu Kitaifa wa THRDC, Onesmo Olengurumwa.
Picha: Pilly Kigome
Mratibu Kitaifa wa THRDC, Onesmo Olengurumwa.

MTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) imepiga kambi ya siku mbili kuwasuka mawakili watetezi wa haki za binadamu kutoka Tanzania Bara na Zanzibar kuwapa elimu kuangalia hali ya kesi zenye maslahi kwa umma, uhuru wa kujieleza na wajibu wa mawakili kwenye mchakato wa uchaguzi na demokrasia.

Mafunzo hayo yanatoa fursa kwa mawakili kushughulikia kesi zenye maslahi kwa umma nchini na kesi za kimkakati na kujadili changamoto zilizopo namna ya kukabiliana nazo wakati wa kuziendesha.

Akizungumza Bagamoyo mkoani Pwani katika ufunguzi wa mafunzo hayo, Mratibu Kitaifa wa THRDC, Onesmo Olengurumwa amesema mtandao huo unalenga kuyafikia makundi mbalimbali katika kuyaelimisha kuhusiana na masuala mazima ya uchaguzi.

Olengurumwa amesema mafunzo hayo yanalenga kuwakumbusha mawakili kuhusiana na wajibu wao, uelewa, kuwaongezea ujuzi zaidi katika kuendesha kesi zenye maslahi kwa umma, kesi za kimkakati, kesi zinazohusu uhuru wa kujieleza, kesi za jinai na kesi zinazohusu masuala ya uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wa 2025.

“THRDC inawajengea uwezo kundi hili kwakuwa ni kundi kubwa na muhimu sana katika jamii ili wasitengue na kwenda kinyume na sheria zilizopo hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi kwakuwa ni wadau wakubwa wa kusimamia demokrasia, haki za binadamu na utawala bora” amesema Olengurumwa.

Aidha amebainisha kuwa kuna mawakili wachache ambao wamebobea katika masuala ya uchaguzi kwa kupitia mafunzo hayo watakwenda kuwaandaa mawakili wa kutosha katika mchakato mzima wa masuala ya uchaguzi.

“Tunataka tufike mahala tnapopataka kama taifa,hivyo tuna wajibu  wa kukumbushana kwakuwa vyombo hivi vipo kwaajili ya kuwatumikia watanzania” amesema