Simba na 'jeshi' la watu 60 Misri

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 06:39 PM Apr 02 2024
Aliyekuwa Kocha wao wa viungo, Adel Zrane.
SIMBA SC
Aliyekuwa Kocha wao wa viungo, Adel Zrane.

HUKU ikiwa katika majonzi ya kumpoteza aliyekuwa Kocha wao wa viungo, Adel Zrane, ambaye ametangulia mbele za haki jana nchini Rwanda, Klabu ya Simba imekwea pipa leo alfajiri kuelekea Misri tayari kwa mchezo wao wa marudiano wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika utakaopigwa Ijumaa wiki hii katika Uwanja wa Kimataifa wa Cairo nchini humo.

Kwa mujibu wa Meneja Habari wa klabu hiyo, Ahmed Ally, walitarajia kuondoka na msafara wa watu 50 hadi 60 kwa ndege ya Shirika la Ndege la Misri na kwenda moja kwa moja hadi nchini humo ambapo leo jioni kikosi cha timu hiyo kitafanya mazoezi yake ya kwanza nchini humo. 

Ahmed alisema katika msafara huo utakuwa na wachezaji 23, viongozi wa benchi la ufundi na viongozi wa Simba pamoja na mashabiki 17 ambao wamejilipia gharama zao wenyewe.

Alisema wanamatumaini makubwa ya kufanya vizuri katika mchezo huo kwa kuwa hata mechi iliyopita ambayo walipoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Al Ahly katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, walimiliki mpira na kucheza vizuri, lakini bahati tu haikuwa upande wao.

Wakati Simba ikieleza hayo, jana serikalini kupitia kwa Naibu Waziri wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamisi Mwinjuma maarufu Mwana FA, alisema klabu hiyo nayo ilipiga hodi serikalini kuomba kupigwa jeki ya kupeleka mashabiki wake nchini Misri kwa ajili ya kuishangilia timu hiyo dhidi ya Al Ahly.

Akizungumza jana akiwa jijini Dodoma, Mwana FA, alisema serikali imepokea maombi ya Klabu ya Simba ya kupeleka mashabiki wake Misri kwa ajili ya kuiunga mkono timu hiyo kwenye mchezo huo wa mkondo wa pili, na maombi hayo yanashughulikiwa.

Hii imekuja siku moja tu baada ya serikali kuwasafirisha mashabiki 48 wa Yanga waliokwenda jijini Pretoria nchini Afrika Kusini kuishangilia timu hiyo itakapocheza mechi yake ya mkondo wa pili dhidi ya Mamelodi Sundowns, Ijumaa wiki hii, mchezo utakaopigwa Uwanja wa Loftus Versfeld, Pretoria.

"Jana (juzi) tumewaaga wapenzi 48 wa Yanga ambao walikuwa wanakwenda Afrika Kusini kwa basi, kushuhudia mchezo wa marudiano kati ya Mamelodi Sundowns na Yanga na baada ya jambo lile, Klabu ya Simba nayo imeleta maombi, ikumbukwe Klabu ya Yanga ilileta maombi mapema na tukafanya kama ambavyo tumelifanya, maombi ya Simba tunayashughulikia na naamini wapenzi wa Klabu ya Simba pia watapata nafasi ya kwenda kuhudhuria mechi kule Misri, kwa hiyo ni jambo tu la kiutaratibu, kwamba serikali inatakiwa kupewa taarifa kuwa klabu inahitaji nini na tuone kama iko ndani ya uwezo wetu kwa wakati huo na tunayafanya. Kwa hiyo nao Simba muda si mrefu watapewa utaratibu na klabu yao," alisema Naibu Waziri huyo.

Pamoja na hayo, Naibu Waziri huyo amesema serikali imewasiliana na mabalozi wa nchi za Misri na Afrika Kusini kuhakikisha timu zote mbili hazipati mkwamo wowote zinapokuwa huko.

"Kama ambavyo unafahamu, mpira una fitna nyingi, lakini nina wasiwasi tabia hizi zipo hasa upande wa huku Kaskazini ambako Simba inakwenda, huko wenyewe mnaita Uarabuni, huku ndiyo kuna tabu kidogo, huku Afrika Kusini hapana, Mamelodi Sundowns siyo Simba wala Yanga kwa Sauzi huko, kwa hiyo sitegemei kama huko watapata kashikashi, lakini ninachoweza kusema balozi zetu zilizopo katika nchi zote mbili zinafanya kazi kwa karibu sana na timu zetu hizi kuhakikisha hakuna mkwamo wowote ule, jicho la serikali liko macho, masikio yako wazi kuhakikisha kwamba hakuna linaloharibika kuelekea michezo hii ya marudiano," alisema.

Katika hatua nyingine, Kocha wa viungo wa zamani wa Klabu ya Simba, Zrane, amefariki dunia jana mchana nchini Rwanda ambako alikuwa akifanya kazi katika Klabu ya APR.

Taarifa zinasema kuwa kocha huyo alifariki dunia ghafla jana saa saba jijini Kigali, huku zingine zikisema kuwa alikutwa amefariki kwenye nyumba aliyokuwa akiishi jijini humo.

Klabu ya APR imethibitisha kifo cha kocha huyo raia wa Tunisia, ambaye mara ya mwisho alionekana katika mchezo wa Jumapili, Machi 31 dhidi ya Rwamagana City wa sare ya bao 1-1 akiwa mzima wa afya.

"Kwa masikitiko makubwa tunatangaza kifo cha kocha wetu wa viungo, Dr, Adel Zrane," ilisema taarifa ya klabu hiyo.

Akiwa nchini, Adel amewahi kuwa kocha wa viungo wa Simba kuanzia mwaka 2018 chini ya Kocha Patrick Aussems na kutimika 2021.

Akiwa Simba, alipata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kushinda makombe matatu ya Ligi Kuu, mataji matatu ya Ngao ya Jamii, makombe mawili ya Azam Sports Federation Cup na Kombe moja la Simba Super Cup.

Mbali na mataji hayo alibaki kuwa kipenzi cha mashabiki na wanachama na klabu hiyo kutokana na kufanya kazi yake kwa bidii, akiwa na mapenzi makubwa na klabu, namna yake ya kushangilia pale timu inapopata bao, lakini pia kazi ya kuwaweka fiti wachezaji, ambapo hadi leo Wanasimba wengi wanaamini hajapatikana mtu sahihi kama yeye.

Klabu ya Simba imesema imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha aliyekuwa kocha wao wa viungo kilichotokea ghafla nchini Rwanda jana mchana.

"Zrane alikuwa mtu mkarimu, mcheshi na rafiki wa wachezaji na alipendwa na kila mmoja kipindi chote alichokuwa katika kikosi chetu tangu, 2018 hadi 2021," ilisema sehemu ya taarifa hiyo huku ikimalizika kwa kutoa pole kwa familia, Klabu ya APR, na wadau wote wa soka kwa msiba huo mzito.