KOCHA Mkuu wa Yanga, Sead Ramovic, amesema ameamua kumtumia beki wake wa kulia, Israel Mwenda kama winga kutokana na kasi aliyonayo ambayo inaweza kuwa na manufaa makubwa kwenye kikosi chake.
Kocha huyo amesema hayo kutokana na kuonekana kuwatumia mabeki wawili upande na kulia, ambao ni Kibwana Shomari na Mwenda mwenyewe kwenye mchezo wa Jumamosi dhidi ya Kagera Sugar, kitu ambacho kimewashangaza wengi, kuanzia mashabiki hadi wachambuzi wa soka, wakiwa hawaelewi lengo ni kuzuia zaidi au kushambilia.
Ramovic, alimpongeza Mwenda kwa dakika chache alizocheza kuwa alifanya vizuri mno na anatarajia atafanya vema zaidi kwenye mechi nyingine zinazokuja.
"Nilimtumia kama winga kutokana na kasi aliyonayo, natamani kuona anawakimbiza wapinzani kwa kasi kupitia pembeni wakisaidiana na mabeki wa pembeni ambao wana uwezo wa kukimbia.
"Natamani kuwa na wachezaji wenye uwezo wa kucheza nafasi zaidi ya moja uwanjani, nikifanikiwa kwenye hilo nitakuwa na urahisi katika machaguo yangu, nampongeza Mwenda kwa dakika chache alizocheza kafanya vizuri," alisema.
Alisema anapenda mno wachezaji ambao muda wote wanatafuta nafasi ya kupenyezewa mpira nyuma ya migongo ya wapinzani, kitu ambacho anaona Mwenda anamudu, hivyo kuendelea kumchezesha nyuma ni kama kumchelewesha.
Hata hivyo, alisema siyo kama amemhamisha kabisa, bali ataendelea kumchezesha kama beki wa kulia au winga kutokana na mahitaji ya timu au mechi husika.
Ulikuwa ni mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu kwa Mwenda kuichezea Yanga tangu asajiliwa kipindi cha dirisha dogo akitokea Singida Black Stars, lakini ukiwa wa pili tangu ajiunge na timu hiyo.
Mchezo wa kwanza ulikuwa ni wa Kombe la FA, ambapo Yanga ilikipiga dhidi ya Copco, ikishinda mabao 5-0, akitoa pasi mbili za mwisho za mabao.
Katika mchezo dhidi ya Kagera Sugar, ambapo timu yake ilishinda mabao 4-0, Mwenda alilazimika kufanyiwa mabadiliko mwanzoni tu mwa kipindi cha pili baada ya kupata majeraha.
Akiuzungumzia mchezo wa keshokutwa dhidi ya KenGold utakaopigwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam, Ramovic, alisema wataingia uwanjani kwa lengo la kuendeleza ubora walionao kwa sasa na kukusanya pointi tatu.
"Lengo letu ni kukusanya pointi tatu kwenye kila mchezo ulio mbele yetu, tunafanya hivyo ili kuhakikisha tunafanikiwa kuubakisha ubingwa wetu," alisema kocha huyo raia wa Ujerumani.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED