KOCHA Mkuu wa Yanga, Sead Ramovic, amesema ameshamaliza kazi ya kuisoma Al Hilal Omdurman ya Sudan na ameweka mipango kabambe namna ya kuikabili kesho kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa katika mechi ya raundi ya kwanza, Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi.
Akizungumza juzi jioni akiwa kwenye maandalizi ya kuelekea kwenye mchezo huo, alisema moja ya sifa ambayo ameiona kwao ni kwamba wako timamu kimwili na wanacheza vizuri, lakini hiyo haimaanishi hawafungiki, na ndiyo maana ametengeneza mipango kwa wachezaji wa safu ya ulinzi, viungo washambuliaji na mastraika jinsi gani ya kudili nao.
Alisema kwa kipindi kifupi ambacho amekabidhiwa timu hawezi kutengeneza kitu kikubwa, zaidi tu ya kuyaangalia makosa na ubora wa wapinzani wao na kuyafanyia kazi.
“Nimewaangalia Al Hilal namna wanavyocheza na najua nini watafanya, timu yao ni ngumu ipo timamu kimwili ila tayari nina mpango namna ya kucheza tunaendelea kufanyia mazoezi mbinu hiyo, nadhani kila kitu kitakaa sawa," alisema Ramovic.
Alisema kikosi chake kipo imara na ana imani wachezaji wake kufanyia kazi kile anachotoa kwenye mazoezi na kupata matokeo mazuri katika mchezo huo wa nyumbani wa Kundi A.
Alisema kazi kubwa aliyonayo ni kuwanoa mabeki wa Yanga wakiongozwa na Bakari Mwamnyeto, Yao Koussi, Dickson Job na Ibrahim Bacca, kuhakikisha wanafanikiwa kuwazuia washambuliaji wa Al Hilal, huku safu ya viungo washambuliaji, kina Clatous Chama, Stephane Aziz wakipeleka mipira mbele na kuwalisha mastraika, Clement Mzize na Prince Dube, ili kila idara ifanye inayokusudiwa kwa ajili ya kusaka ushindi wa kwanza.
Siku chache nyuma, Kocha Mkuu wa Al Hilal, Florent Ibenge, alisema ujio wa Ramovic kwenye kikosi cha Yanga umewachanganya kwani walikuwa wamejipanga kucheza kikosi cha mfumo wa Miguel Gamondi, lakini kuondoka kwake kumewaathiri kwa kuwa hawajui kocha huyo atacheza mfumo gani ingawa atalifanyia kazi hilo.
"Tulishamjua Gamondi aina yake ya uchezaji na mifumo, tulifanyia kazi namna timu yake inavyocheza, huyu mpya kwetu itakuwa ni mgumu sana, hatujui lolote, hatujui atakuja na mbinu gani. Tunatakiwa kuwa makini sana," alisema Ibenge.
Yanga itakutana na Al Hilal Omdurman ukiwa ni mchezo wa saba tangu timu hizo zilipokutana kwa mara ya kwanza mwaka 1988.
Yanga imeshinda mara mbili kati ya hizo kama ilivyo kwa Wasudan hao, huku zikitoka sare mara mbili pia.
Mara ya mwisho timu hizo kukutana ilikuwa ni Oktoba 16, 2022 kwenye mechi ya raundi ya kwanza nchini Sudan, Al Hilal ikishinda bao 1-0 na kusonga mbele hatua ya makundi, baada ya mchezo wa kwanza uliochezwa Oktoba 8, mwaka 2022, timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1.
Kabla ya hapo, timu hizo zilikutana mara ya kwanza Januari 3, 1988, Al Hilal ikishinda mabao 2-0 katika hatua ya makundi ya Kombe la Afrika Mashariki na Kati (Kagame Cup), na Januari 10, 1992, kwenye michuano hiyo hiyo, Yanga ilishinda kwa mikwaju 10-9 ya penalti katika mchezo wa nusu fainali baada ya suluhu ya dakika 90.
Kisha Yanga ikaenda kucheza fainali dhidi ya Simba, Zanzibar na kufungwa kwa mikwaju ya penalti, Mohamed Mwameja wakati huo aliyejiunga nayo akitokea Coastal Union, akiokoa mbili.
Mwaka 1994, mechi iliyochezwa Januari 7, Yanga na Al Hilal zilitoka sare ya bao 1-1 katika hatua za makundi, Kombe la Afrika Mashariki na kati, na Januari 10, 1999, Yanga iliichapa Al Hilal mabao 2-1 katika mchezo wa robo fainali.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED