NAIBU Waziri wa Utamaduni,Sanaa na Michezo Hamis Mwinjuma,amezindua Rasmi ligi ya Dr.Samia/ Katambi Cup ambayo imelenga kuibua vipaji vya vijana, na itashirikisha timu 32 za mpira wa miguu.
Ligi hiyo imezinduliwa jana katika viwanja vya Jasco vilivyopo Ngokolo, na kuchezwa michezo mbalimbali ikiwamo ya kuvuta kamba,kukimbiza kuku,kuchoma nyama ambapo washindi waliibuka na zawadi, ambapo timu hizo 32 za mpira wa miguu zitatimua vumbi katika viwanja mbalimbali.
Naibu Waziri Mwinjuma akizungumza wakati wa uzinduzi wa ligi hiyo, amempongeza Mbunge Katambi kwa kuibua vipaji vya vijana sababu kwa sasa mpira ni ajira, huku akiwaomba wananchi wa Shinyanga kwamba wasije jaribu kumpoteza mbunge huyo bali wanapaswa kumlinda na kumpigania kwa nguvu zote ili aendelee kuwa mbunge wao na kuwaletea maendeleo.
“Rais wetu Mheshimiwa Dk. Samia Suluhu Hassan anapenda michezo hivyo Katambi kuanzisha Ligi hii ni kumuunga mkono Rais katika kukuza michezo hapa nchini na kutoa ajira kwa vijana,”amesema Mwinjuma.
“Katambi ni Mbunge ambaye anachapa kazi, ni mtu mwenye maarifa makubwa sana, hata Rais Samia ana mwamini katika kumsaidia kazi na kuwatumikia Watanzania wote,hivyo anapaswa kulinda na kupiganiwa wabunge kama hawa wapo wachache msije kumpoteza,”ameongeza
Aidha,ametaja zawadi ambazo watapewa washindi kwenye ligi hiyo kwamba mshindi wa kwanza wa mpira wa miguu atapewa kiasi cha Sh.milioni 6 pamoja na kombe,mpira na jezi, mshindi wa pili atapewa Sh.milioni 3, kombe,mpira na jezi, huku mshindi wa tatu atapewa Sh.milioni moja ,mpira na jezi.
Ametaja zawadi zingine kwamba mfungaji bora atapewa Sh. Elfu 50, mchezaji mwenye nidhamu Sh.laki moja, na washindi wa kucheza “Dansi”mshindi wa kwanza atapewa Sh.milioni Moja, wapili Laki 5 na watatu Laki 3, na kueleza kwamba zawadi ambazo ametoa mbunge huyo ni fedha nyingi na anawapenda wananchi wake.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha, akizungumza kwenye uzinduzi huo amempongeza Mbunge Katambi kwa kuanzisha ligi hiyo, na kubainisha kwamba michezo inaleta umoja, kuimarisha afya na hata kutoa ajira kwa vijana.
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Shinyanga Mjini Anold Makombe alisema Mbunge Katambi anaitekeleza vyema ilani ya uchaguzi ya CCM kwa vitendo sababu hata michezo ipo kwenye ilani hiyo.
Naye Mbunge wa Shinyanga Mjini Patrobas Katambi ambaye pia ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu,kazi,vijana,ajira na watu wenye ulemavu, amesema lengo la ligi hiyo ni kuibua vipaji vya vijana, ambao watapata ajira kwenye timu mbalimbali ikiwamo na Stand united ambayo wapo kwenye mikakati ya kuipandisha kushiriki kucheza Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED