MIONGONI mwa taasisi zinazonufaika na program ya kujenga Mfumo Endelevu wa Kupambana na Rushwa Tanzania(BSAAT) ni Wizara ya Katiba na Sheria.
Programu hiyo inatekelezwa na Wizara kwa ushirikiano na Idara maalum inayoratibu na kusimamia programu hiyo kutoka Ofisi ya Rais Ikulu kupitia ufadhili wa Serikali ya Uingereza.
Lengo la programu ni kuzijengea uwezo Taasisi za umma katika kupambana na rushwa Tanzania.
Katika Programu hiyo, Wizara inatekeleza shughuli zinazohusiana na maboresho ya mfumo wa haki jinai hususani kuboresha maeneo ya kisera, kisheria na ushughulikiaji wa mashauri ya rushwa.
Moja ya majukumu ambayo yametekelezwa na Wizara kupitia programu ya BSAAT ni pamoja na uanzishwaji wa Kituo cha Huduma kwa Mteja kwa ajili ya kupokea malalamiko na taarifa za rushwa kubwa.
Akizungumza kuhusu mafanikio yaliyopatikana tangu kuanza kufanya kazi kituo hicho Februari 21 mwaka huu, Mkurugenzi wa Idara ya Katiba na Ufuatiliaji Haki wa Wizara hiyo, Jane Lyimo, anasema kituo hicho kimeanza kazi baada ya kukamilisha usimikaji wa mifumo na vifaa mbalimbali vya kiteknolojia ya kisasa.
“Tangu kuanzishwa kwake, Kituo kimeendelea kupokea malalamiko ya wananchi kutoka maeneo mbalimbali nchini. Huduma ya kituo hutolewa na wataalamu wa sheria waliojengewa uwezo katika kutoa huduma kwa wananchi,”anasema
Anafafanua kuwa malalamiko ya rushwa kubwa yanayopokelewa huwasilishwa kwa mamlaka husika (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)) kama rufaa kwa ajili ya uchunguzi na baadae hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi ya mhusika pindi inapobainika pasipo shaka kuwa amehusika na tuhuma za rushwa kama ilivyowasilishwa.
Anasema pamoja na masuala ya malalamiko yanayohusu rushwa kituo hupokea malalamiko yanayohusu masuala ya kisheria.
“Huduma nyingine zinazotolewa na kituo ni Msaada wa Kisheria kwa wasiomudu gharama za wanasheria; kupokea maoni, mapendekezo na ushauri juu ya huduma mbalimbali zinazotolewa na Wizara,”anasema.
MAFANIKIO YA KITUO
Lyimo anasema kituo hicho kimepokea simu 6987 pamoja na jumbe mbalimbali kupitia mitandao ya kijamii kupitia namba maalum ambayo ni 026 216 0360, Whatsapp 0739101910 na barua pepe [email protected]
Anabainisha kuwa mbali na kufanyia kazi masuala yanayohusu rushwa kubwa, kituo kinapokea malalamiko mbalimbali yanayohusu masuala ya kisheria na yasiyo ya kisheria na kuyashughulikia ipasavyo.
“Kwa kipindi cha mwezi Februari hadi Novemba, 2024 Kituo kimepokea malalamiko 663, kati ya hayo malalamiko 561 yameshughulikiwa kwa ukamilifu na malalamiko 102 yako katika hatua mbalimbali za utekelezaji wake,”anasema.
Anaeleza kuwa kati ya simu zilizopigwa nyingine zilihusisha maulizo, ushauri, na masuala ambayo yanahitaji ufafanuzi wa papo kwa hapo na mrejesho kutoka kwa maafisa wanaotoa huduma.
Aidha, anasema malalamiko yaliyosajiliwa na kushughulikiwa kikamilifu na yanayoendelea kushughulikiwa kutoka mikoa mbalimbali nchini.
MAFUNZO KWA WATUMISHI
Anasema watumishi wa Wizara na baadhi kutoka taasisi zenye uhusiano na shughuli za mfumo wamepatiwa mafunzo yanayolenga kuwajengea uelewa kuhusu uwapo na madhumuni ya Kituo hicho.
“Kuwajenga uelewa wa namna ya kupokea malalamiko yanayowasilishwa na wananchi na kuyafanyia kazi; Namna ya kutumia mifumo iliyosimikwa kwa ajili ya utoaji wa Huduma (Kupokea na kujibu simu, uhifadhi wa taarifa n.k),”anasema
Anasema mafunzo mengine ni namna bora ya kuhudumia wateja na kuwajengea uwezo wa kuhakikisha Kituo cha Huduma kwa Mteja kinafanya kazi kwa lengo lililokusudiwa kulingana na mpango wa kuanzishwa kwake.
“Mafunzo haya ni endelevu kwa maafisa wanaotoa huduma katika kituo na baadhi ya maafisa viungo wa taasisi mbalimbali ambao taasisi zao zina uhusiano na huduma zinazotolewa na mfumo,”anasema.
ALICHOSEMA PROF.KABUDI
Akizindua kituo hicho Septemba 5, 2024, Waziri wa Katiba na Sheria, Prof. Palamagamba Kabudi akiwa ameambatana na Naibu Waziri Jumanne Sagini, anasema wananchi wamekuwa na mwamko mkubwa wa kuwasilisha malalamiko na hoja zao kisheria ili zipatiwe ufumbuzi wa haraka.
Anasema mwamko huo umeonekana kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (Mama Samia Legal Aid Campaign), ambayo hadi sasa imefika mikoa ya Dodoma, Manyara, Singida, Simiyu, Shinyanga, Ruvuma na Njombe imechochea kuanzishwa kwa kituo hicho.
Prof.Kabudi anasema serikali imeanzisha kituo hicho baada ya kubaini wananchi wamekuwa wakiwasilisha malalamiko mengi kwa njia ya barua na wengine wakitumia gharama kubwa kusafiri kuyapeleka wizarani Dodoma.
“Kituo hichi ni utekelezaji wa falsafa ya R nne za Rais Samia Suluhu Hassan ambazo ni Maridhiano, Ustahimilivu, Mabadiliko na Kujenga upya, kupitia falsafa hizi wizara inawezesha utatuzi wa migogoro, inatoa elimu na msaada wa kisheria,”anasema.
Anaongeza “Hii imesaidia kwa wananchi wasio na uwezo wa kumudu gharama za usafiri kuja kuwasilisha malalamiko yao wizarani, kwasasa wananchi walio maeneo ya mbali sasa wana uwezo kuwasilisha malalamiko yao kwa njia ya simu kwenye kituo hichi na kufanyiwa kazi bila kufika wizarani.”
Anawakaribisha wananchi kukitumia kituo hicho kuwasilisha malalamiko mbalimbali yanayowakabili, kwa kuwa Wizara imejipanga vizuri kushughulikia malalamiko hayo kisheria.
“Tunakaribisha uwasilishaji wa taarifa au malalamiko yoyote kuhusu rushwa. Tunakuhakikishia kila mwananchi atakayewasilisha suala/ lalamiko hilo litafanyiwa kazi ipasavyo na mwananchi husika kupatiwa mrejesho wa utekelezaji wake,”anasema.
Vilevile, anasema Wizara itaendelea kushirikiana na taasisi nufaika na programu ya BSAAT katika kufanya kazi ili kubadilishana uzoefu wa namna bora ya utekelezaji wake ili kufikia lengo lililokusudiwa.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED